Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mika 4:1-13

Mika 4:1-13 Biblia Habari Njema (BHN)

Utakuja wakati ambapo mlima wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu utakuwa mkubwa kuliko milima yote. Naam, utakwezwa juu ya vilima vyote. Watu wengi watamiminika huko, mataifa mengi yataujia na kusema: “Twendeni juu kwenye mlima wa Mwenyezi-Mungu, twende katika nyumba ya Mungu wa Yakobo, ili atufundishe njia zake, nasi tufuate nyayo zake. Maana mwongozo utatoka huko Siyoni; neno la Mwenyezi-Mungu huko Yerusalemu.” Mungu atasuluhisha mizozo ya mataifa mengi, atakata mashauri ya mataifa makubwa ya mbali. Nayo yatafua mapanga yao kuwa majembe, na mikuki yao kuwa miundu ya kupogolea. Taifa halitapigana na taifa lingine, wala hayatafanya tena mazoezi ya vita. Kila mtu atakaa kwa amani chini ya mitini na mizabibu yake, bila kutishwa na mtu yeyote. Mwenyezi-Mungu wa majeshi, ametamka yeye mwenyewe. Mataifa mengine hufuata njia zao, kwa kuitegemea miungu yao, lakini sisi twafuata njia zetu kwa kumtegemea Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, milele na milele. Mwenyezi-Mungu asema, “Siku ile nitawakusanya walemavu, naam, nitawakusanya waliochukuliwa uhamishoni, watu wale ambao niliwaadhibu. Hao walemavu ndio watakaobaki hai; hao waliochukuliwa uhamishoni watakuwa taifa lenye nguvu. Nami Mwenyezi-Mungu nitawatawala mlimani Siyoni, tangu wakati huo na hata milele.” Nawe kilima cha Yerusalemu, wewe ngome ya Siyoni, ambamo Mungu anafanya ulinzi juu ya watu wake, kama mchungaji juu ya kondoo wake; wewe utakuwa tena mji maarufu kama hapo awali, Yerusalemu utakuwa tena mji mkuu wa mfalme. Sasa kwa nini mnalia kwa sauti? Je, hamna mfalme tena? Mshauri wenu ametoweka? Mnapaza sauti ya uchungu, kama mama anayejifungua! Enyi watu wa Siyoni, lieni na kugaagaa kama mama anayejifungua! Maana sasa mtaondoka katika mji huu mwende kukaa nyikani, mtakwenda mpaka Babuloni. Lakini huko, mtaokolewa. Huko Mwenyezi-Mungu atawakomboa makuchani mwa adui zenu. Mataifa mengi yamekusanyika kuwashambulia. Yanasema: “Acheni mji wao utiwe najisi, nasi tuyaone magofu ya Siyoni!” Lakini wao hawafahamu mawazo ya Mwenyezi-Mungu wala hawaelewi mpango wake: Kwamba amewakusanya pamoja, kama miganda mahali pa kupuria. Mwenyezi-Mungu asema, “Enyi watu wa Siyoni, inukeni mkawaadhibu adui zenu! Nitawapeni nguvu kama fahali mwenye pembe za chuma na kwato za shaba. Mtawasaga watu wa mataifa mengi; mapato yao mtaniwekea wakfu mimi, mali zao mtanitolea mimi Bwana wa dunia yote.”

Shirikisha
Soma Mika 4

Mika 4:1-13 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Lakini itakuwa katika siku za mwisho, ya kwamba mlima wa nyumba ya BWANA utawekwa imara juu ya milima, nao utainuliwa juu ya vilima; na watu wa mataifa watauendea makundi makundi. Na mataifa mengi watakwenda na kusema, Njooni, twende juu mlimani kwa BWANA, na nyumbani kwa Mungu wa Yakobo; naye atatufundisha njia zake, nasi tutakwenda katika mapito yake; kwa maana katika Sayuni itatoka sheria, na neno la BWANA litatoka Yerusalemu. Naye atafanya hukumu kati ya watu wa kabila nyingi, naye atawakemea mataifa wenye nguvu walio mbali; nao watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao iwe miundu; taifa halitainua upanga juu ya taifa lingine, wala hawatajifunza vita tena kamwe. Bali wataketi kila mtu chini ya mzabibu wake, na chini ya mtini wake; wala hapana mtu atakayewatia hofu; kwa kuwa kinywa cha BWANA wa majeshi kimesema hivi. Kwa maana mataifa yote watakwenda, kila moja kwa jina la mungu wake, na sisi tutakwenda kwa jina la BWANA, Mungu wetu, milele na milele. Katika siku ile, asema BWANA, nitamkusanya yeye achechemeaye, nami nitamrudisha yeye aliyefukuzwa, na yeye niliyemtesa. Nami nitamfanya yeye aliyechechemea kuwa mabaki, na yeye aliyetupwa mbali kuwa taifa lenye nguvu, na BWANA atawamiliki katika mlima Sayuni tangu sasa na hata milele. Na wewe, Ee mnara wa kundi, kilima cha binti Sayuni, utajiliwa; naam, mamlaka ya kwanza yatakuja, ufalme wa binti Yerusalemu. Sasa mbona unapiga kelele? Je! Hakuna mfalme kwako, mshauri wako amepotea, hata umeshikwa na uchungu kama mwanamke wakati wa kuzaa? Uwe na uchungu, utaabike ili uzae, Ee binti Sayuni, kama mwanamke mwenye uchungu; maana sasa utatoka mjini, nawe utakaa katika mashamba; utafika hata Babeli; huko ndiko utakakookolewa; huko ndiko BWANA atakakokukomboa kutoka kwa mikono ya adui zako. Na sasa mataifa mengi wamekusanyika juu yako, wasemao, Na atiwe unajisi; macho yetu na yaone shari ya Sayuni. Lakini wao hawayajui mawazo ya BWANA, wala hawafahamu shauri lake; kwamba amewakusanya kama miganda mahali pa kupuria. Haya, simama upure, Ee binti Sayuni; kwa maana nitafanya pembe yako kuwa chuma, na kwato zako kuwa shaba; nawe utapondaponda mataifa mengi, na faida yao utaiweka wakfu kwa BWANA, na mali zao kwa BWANA wa dunia yote.

Shirikisha
Soma Mika 4

Mika 4:1-13 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Lakini itakuwa katika siku za mwisho, ya kwamba mlima wa nyumba ya BWANA utawekwa imara juu ya milima, nao utainuliwa juu ya vilima; na watu wa mataifa watauendea makundi makundi. Na mataifa mengi watakwenda na kusema, Njoni, twende juu mlimani kwa BWANA, na nyumbani kwa Mungu wa Yakobo; naye atatufundisha njia zake, nasi tutakwenda katika mapito yake; kwa maana katika Sayuni itatoka sheria, na neno la BWANA litatoka Yerusalemu. Naye atafanya hukumu kati ya watu wa kabila nyingi, naye atawakemea mataifa wenye nguvu walio mbali; nao watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao iwe miundu; taifa halitainua upanga juu ya taifa lingine, wala hawatajifunza vita tena kamwe. Bali wataketi kila mtu chini ya mzabibu wake, na chini ya mtini wake; wala hapana mtu atakayewatia hofu; kwa kuwa kinywa cha BWANA wa majeshi kimesema hivi. Kwa maana mataifa yote watakwenda, kila moja kwa jina la mungu wake, na sisi tutakwenda kwa jina la BWANA, Mungu wetu, milele na milele. Katika siku ile, asema BWANA, nitamkusanya yeye achechemeaye, nami nitamrudisha yeye aliyefukuzwa, na yeye niliyemtesa. Nami nitamfanya yeye aliyechechemea kuwa mabaki, na yeye aliyetupwa mbali kuwa taifa lenye nguvu, na BWANA atawamiliki katika mlima Sayuni tangu sasa na hata milele. Na wewe, Ee mnara wa kundi, kilima cha binti Sayuni, utajiliwa; naam, mamlaka ya kwanza yatakuja, ufalme wa binti Yerusalemu. Sasa mbona unapiga kelele? Je! Hakuna mfalme kwako, mshauri wako amepotea, hata umeshikwa na utungu kama mwanamke wakati wa kuzaa? Uwe na utungu, utaabike ili uzae, Ee binti Sayuni, kama mwanamke mwenye utungu; maana sasa utatoka mjini, nawe utakaa katika mashamba; utafika hata Babeli; huko ndiko utakakookolewa; huko ndiko BWANA atakakokukomboa katika mikono ya adui zako. Na sasa mataifa mengi wamekusanyika juu yako, wasemao, Na atiwe unajisi; macho yetu na yaone shari ya Sayuni. Lakini wao hawayajui mawazo ya BWANA, wala hawafahamu shauri lake; kwa maana amewakusanya kama miganda sakafuni. Haya, simama upure, Ee binti Sayuni; kwa maana nitafanya pembe yako kuwa chuma, na kwato zako kuwa shaba; nawe utaponda-ponda mataifa mengi, na faida yao utaiweka wakfu kwa BWANA, na mali zao kwa BWANA wa dunia yote.

Shirikisha
Soma Mika 4

Mika 4:1-13 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Katika siku za mwisho mlima wa Hekalu la BWANA utaimarishwa kama mlima mkuu miongoni mwa milima yote; utainuliwa juu ya vilima, na watu wa mataifa watamiminika humo. Mataifa mengi yatakuja na kusema, “Njooni, twendeni mlimani mwa BWANA, kwenye nyumba ya Mungu wa Yakobo. Atatufundisha njia zake, ili tuweze kuenenda katika mapito yake.” Sheria itatoka Sayuni, neno la BWANA litatoka Yerusalemu. Atahukumu kati ya mataifa mengi, na ataamua migogoro ya mataifa yenye nguvu na yaliyo mbali. Watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao kuwa miundu ya kukata matawi. Taifa halitainua upanga dhidi ya taifa jingine, wala hawatajifunza vita tena. Kila mtu ataketi chini ya mzabibu wake na chini ya mtini wake, wala hakuna mtu atakayewaogopesha, kwa kuwa BWANA Mwenye Nguvu Zote amesema. Mataifa yote yanaweza kutembea katika jina la miungu yao; sisi tutatembea katika jina la BWANA Mungu wetu milele na milele. BWANA “Katika siku hiyo,” asema BWANA, “nitawakusanya walemavu; nitawakusanya walio uhamishoni na wale niliowahuzunisha. Nitawafanya walemavu kuwa mabaki, wale waliofukuzwa kuwa taifa lenye nguvu. BWANA atatawala juu yao katika Mlima Sayuni kuanzia siku hiyo na hata milele. Lakini kuhusu wewe, ee mnara wa ulinzi wa kundi, ee ngome ya Binti Sayuni, milki ya awali itarudishwa kwako, ufalme utakuja kwa Binti Yerusalemu.” Kwa nini sasa unalia kwa nguvu: kwani huna mfalme? Je, mshauri wako amekufa, hata maumivu yakukamate kama ya mwanamke aliye na utungu wa kuzaa? Gaagaa kwa utungu, ee Binti Sayuni, kama mwanamke mwenye utungu wa kuzaa, kwa kuwa sasa ni lazima uuache mji ukapige kambi uwanjani. Utakwenda Babeli; huko utaokolewa. Huko BWANA atakukomboa kutoka mikononi mwa adui zako. Lakini sasa mataifa mengi yamekusanyika dhidi yako. Wanasema, “Mwache anajisiwe, macho yetu na yatazame Sayuni kwa furaha!” Lakini hawayajui mawazo ya BWANA; hawauelewi mpango wake, yeye awakusanyaye kama miganda kwenye sakafu ya kupuria. “Inuka upure, ee Binti Sayuni, kwa kuwa nitakupa pembe za chuma; nitakupa kwato za shaba na utavunja vipande vipande mataifa mengi.”

Shirikisha
Soma Mika 4