Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mathayo 3:2-17

Mathayo 3:2-17 BHN

“Tubuni, maana ufalme wa mbinguni umekaribia.” Huyu Yohane ndiye yule ambaye nabii Isaya alinena juu yake aliposema: “Sauti ya mtu anaita jangwani: ‘Mtayarishieni Bwana njia yake, nyosheni barabara zake.’” Yohane alivaa vazi lililoshonwa kwa manyoya ya ngamia, na ukanda wa ngozi kiunoni mwake. Chakula chake kilikuwa nzige na asali ya mwituni. Basi, watu kutoka Yerusalemu, kutoka pande zote za Yudea na sehemu zote za kandokando ya mto Yordani, walimwendea, wakaziungama dhambi zao, naye akawabatiza katika mto Yordani. Lakini alipowaona Mafarisayo wengi na Masadukayo wanamjia ili awabatize, aliwaambia, “Enyi kizazi cha nyoka! Ni nani aliyewadokezea muikimbie ghadhabu inayokuja? Onesheni kwa vitendo kwamba mmetubu. Msifikiri na kujisemea, ‘Baba yetu ni Abrahamu!’ Nawaambieni hakika, Mungu anaweza kuyafanya mawe haya yawe watoto wa Abrahamu. Basi, shoka liko tayari kwenye mizizi ya miti; hivyo, kila mti usiozaa matunda mazuri utakatwa na kutupwa motoni. Mimi ninawabatizeni kwa maji kuonesha mmetubu. Lakini anayekuja baada yangu ana nguvu kuliko mimi, nami sistahili hata kubeba viatu vyake. Yeye atawabatizeni kwa Roho Mtakatifu na kwa moto. Yeye anashika mkononi chombo cha kupuria nafaka, ili aipure nafaka yake; akusanye ngano yake ghalani, na makapi ayachome kwa moto usiozimika.” Wakati huo Yesu alitoka Galilaya akafika katika mto Yordani, akamwendea Yohane ili abatizwe naye. Lakini Yohane alijaribu kumzuia akisema, “Je, wewe unakuja kwangu? Mimi hasa ndiye ninayehitaji kubatizwa nawe.” Lakini Yesu akamjibu, “Acha tu iwe hivyo kwa sasa, maana ndivyo inavyofaa tuyatekeleze yale yote Mungu anayotaka.” Hapo Yohane akakubali. Mara tu Yesu alipokwisha batizwa, alitoka majini; na kumbe mbingu zikafunguka, akaona Roho wa Mungu akishuka kama njiwa na kutua juu yake. Sauti kutoka mbinguni ikasema, “Huyu ndiye Mwanangu mpendwa, nimependezwa naye.”

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Mathayo 3:2-17