Mathayo 3:2-17
Mathayo 3:2-17 Biblia Habari Njema (BHN)
“Tubuni, maana ufalme wa mbinguni umekaribia.” Huyu Yohane ndiye yule ambaye nabii Isaya alinena juu yake aliposema: “Sauti ya mtu anaita jangwani: ‘Mtayarishieni Bwana njia yake, nyosheni barabara zake.’” Yohane alivaa vazi lililoshonwa kwa manyoya ya ngamia, na ukanda wa ngozi kiunoni mwake. Chakula chake kilikuwa nzige na asali ya mwituni. Basi, watu kutoka Yerusalemu, kutoka pande zote za Yudea na sehemu zote za kandokando ya mto Yordani, walimwendea, wakaziungama dhambi zao, naye akawabatiza katika mto Yordani. Lakini alipowaona Mafarisayo wengi na Masadukayo wanamjia ili awabatize, aliwaambia, “Enyi kizazi cha nyoka! Ni nani aliyewadokezea muikimbie ghadhabu inayokuja? Onesheni kwa vitendo kwamba mmetubu. Msifikiri na kujisemea, ‘Baba yetu ni Abrahamu!’ Nawaambieni hakika, Mungu anaweza kuyafanya mawe haya yawe watoto wa Abrahamu. Basi, shoka liko tayari kwenye mizizi ya miti; hivyo, kila mti usiozaa matunda mazuri utakatwa na kutupwa motoni. Mimi ninawabatizeni kwa maji kuonesha mmetubu. Lakini anayekuja baada yangu ana nguvu kuliko mimi, nami sistahili hata kubeba viatu vyake. Yeye atawabatizeni kwa Roho Mtakatifu na kwa moto. Yeye anashika mkononi chombo cha kupuria nafaka, ili aipure nafaka yake; akusanye ngano yake ghalani, na makapi ayachome kwa moto usiozimika.” Wakati huo Yesu alitoka Galilaya akafika katika mto Yordani, akamwendea Yohane ili abatizwe naye. Lakini Yohane alijaribu kumzuia akisema, “Je, wewe unakuja kwangu? Mimi hasa ndiye ninayehitaji kubatizwa nawe.” Lakini Yesu akamjibu, “Acha tu iwe hivyo kwa sasa, maana ndivyo inavyofaa tuyatekeleze yale yote Mungu anayotaka.” Hapo Yohane akakubali. Mara tu Yesu alipokwisha batizwa, alitoka majini; na kumbe mbingu zikafunguka, akaona Roho wa Mungu akishuka kama njiwa na kutua juu yake. Sauti kutoka mbinguni ikasema, “Huyu ndiye Mwanangu mpendwa, nimependezwa naye.”
Mathayo 3:2-17 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia. Kwa sababu huyo ndiye aliyenenwa na nabii Isaya, akisema, Sauti ya mtu aliaye nyikani, Itengenezeni njia ya Bwana, Yanyosheni mapito yake. Naye Yohana mwenyewe alikuwa na vazi lake la singa za ngamia, na mshipi wa ngozi kiunoni mwake; na chakula chake kilikuwa nzige na asali ya mwitu. Ndipo walipomwendea Yerusalemu, na Uyahudi wote, na nchi zote za kandokando ya Yordani; naye akawabatiza katika mto wa Yordani, huku wakiziungama dhambi zao. Hata alipoona wengi miongoni mwa Mafarisayo na Masadukayo wakiujia ubatizo wake, aliwaambia, Enyi wazao wa nyoka, ni nani aliyewaonya ninyi kuikimbia hasira itakayokuja? Basi zaeni matunda yapasayo toba; wala msiwaze mioyoni mwenu kwamba, Tunaye baba, ndiye Ibrahimu; kwa maana nawaambia ya kwamba Mungu aweza katika mawe haya kumwinulia Ibrahimu watoto. Na shoka limekwisha kuwekwa penye mashina ya miti; basi kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni. Kweli mimi nawabatiza kwa maji kwa ajili ya toba; bali yeye ajaye nyuma yangu ana nguvu kuliko mimi, wala sistahili hata kuvichukua viatu vyake; yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto. Ambaye pepeto lake li mkononi mwake, naye atausafisha sana uwanda wake; na kuikusanya ngano yake ghalani, bali makapi atayateketeza kwa moto usiozimika. Wakati huo Yesu akaja kutoka Galilaya mpaka Yordani kwa Yohana ili abatizwe. Lakini Yohana alitaka kumzuia, akisema, Mimi nahitaji kubatizwa na wewe, nawe waja kwangu? Yesu akajibu akamwambia, Kubali hivi sasa; kwa kuwa ndivyo itupasavyo kuitimiza haki yote. Basi akamkubali. Naye Yesu alipokwisha kubatizwa mara akapanda kutoka majini; na tazama, mbingu zikamfunukia, akamwona Roho wa Mungu akishuka kama hua, akija juu yake; na tazama, sauti kutoka mbinguni ikisema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye.
Mathayo 3:2-17 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia. Kwa sababu huyo ndiye aliyenenwa na nabii Isaya, akisema, Sauti ya mtu aliaye nyikani, Itengenezeni njia ya Bwana, Yanyosheni mapito yake. Naye Yohana mwenyewe alikuwa na vazi lake la singa za ngamia, na mshipi wa ngozi kiunoni mwake; na chakula chake kilikuwa nzige na asali ya mwituni. Ndipo walipomwendea wa Yerusalemu, na wa Yudea wote, na nchi zote za kandokando ya Yordani; naye akawabatiza katika mto wa Yordani, huku wakiziungama dhambi zao. Na alipoona wengi miongoni mwa Mafarisayo na Masadukayo wakiujia ubatizo wake, aliwaambia, Enyi wazawa wa nyoka, ni nani aliyewaonya ninyi kuikimbia hasira itakayokuja? Basi zaeni matunda yapasayo toba; wala msiwaze mioyoni mwenu kwamba, Tunaye baba, ndiye Abrahamu; kwa maana nawaambia ya kwamba Mungu aweza katika mawe haya kumwinulia Abrahamu watoto. Na shoka limekwisha kuwekwa penye mashina ya miti; basi kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni. Kweli mimi nawabatiza kwa maji kwa ajili ya toba; bali yeye ajaye nyuma yangu ana nguvu kuliko mimi, wala sistahili hata kuvichukua viatu vyake; yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto. Ambaye pepeto lake li mkononi mwake, naye atausafisha sana uwanda wake; na kuikusanya ngano yake ghalani, bali makapi atayateketeza kwa moto usiozimika. Wakati huo Yesu akaja kutoka Galilaya mpaka Yordani kwa Yohana ili abatizwe. Lakini Yohana alitaka kumzuia, akisema, Mimi nahitaji kubatizwa na wewe, nawe waja kwangu? Yesu akajibu akamwambia, Kubali hivi sasa; kwa kuwa ndivyo itupasavyo kuitimiza haki yote. Ndipo akakubali. Naye Yesu alipokwisha kubatizwa mara aliibuka kutoka majini na tazama, mbingu zikamfunukia, akamwona Roho wa Mungu akishuka kama hua, na kutua juu yake; na tazama, sauti kutoka mbinguni ikasema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye.
Mathayo 3:2-17 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
“Tubuni, kwa maana Ufalme wa Mbinguni umekaribia.” Huyu ndiye yule aliyenenwa habari zake na nabii Isaya aliposema: “Sauti ya mtu aliaye huko nyikani, ‘Tayarisheni njia kwa ajili ya Bwana, yanyoosheni mapito yake.’ ” Basi Yohana alivaa mavazi yaliyotengenezwa kwa singa za ngamia, akiwa na mkanda wa ngozi kiunoni mwake. Chakula chake kilikuwa nzige na asali ya mwitu. Watu walikuwa wakimwendea kutoka Yerusalemu, Uyahudi yote na nchi zote za kandokando ya Mto Yordani. Nao wakaziungama dhambi zao, akawabatiza katika Mto Yordani. Lakini alipowaona Mafarisayo na Masadukayo wengi wakija ili kubatizwa, aliwaambia: “Ninyi watoto wa nyoka! Ni nani aliyewaonya kuikimbia ghadhabu inayokuja? Basi zaeni matunda yastahiliyo toba. Wala msidhani mnaweza kusema mioyoni mwenu kuwa, ‘Sisi tunaye Abrahamu, baba yetu.’ Nawaambia kuwa Mungu anaweza kumwinulia Abrahamu watoto kutoka kwa mawe haya. Hata sasa shoka limeshawekwa tayari kwenye shina la kila mti, basi kila mti usiozaa matunda mazuri, hukatwa na kutupwa motoni. “Mimi nawabatiza kwa maji kwa ajili ya toba. Lakini nyuma yangu anakuja yeye aliye na uwezo kuliko mimi, ambaye sistahili hata kuvichukua viatu vyake. Yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto. Pepeto lake liko mkononi mwake, naye atasafisha sakafu yake ya kupuria, na kuikusanya ngano ghalani na kuyateketeza makapi kwa moto usiozimika.” Kisha Yesu akaja kutoka Galilaya mpaka Mto Yordani ili Yohana ambatize. Lakini Yohana akajitahidi kumzuia, akimwambia, “Mimi ninahitaji kubatizwa na wewe, nawe waja kwangu nikubatize?” Lakini Yesu akamjibu, “Kubali hivi sasa, kwa maana ndivyo itupasavyo kwa njia hii kuitimiza haki yote.” Hivyo Yohana akakubali. Naye Yesu alipokwisha kubatizwa, mara alipotoka ndani ya maji, ghafula mbingu zikafunguka, akamwona Roho wa Mungu akishuka kama hua na kutulia juu yake. Nayo sauti kutoka mbinguni ikasema, “Huyu ni Mwanangu mpendwa, ambaye ninapendezwa sana naye.”