Mathayo 27:32-66
Mathayo 27:32-66 BHN
Walipokuwa wakienda, wakamkuta mtu mmoja jina lake Simoni, mwenyeji wa Kurene, wakamlazimisha kuuchukua msalaba wake Yesu. Walipofika mahali paitwapo Golgotha, maana yake, mahali pa Fuvu la Kichwa, wakampa mchanganyiko wa divai na kitu kichungu. Lakini Yesu alipoonja akakataa kunywa. Walimsulubisha, kisha wakagawana mavazi yake kwa kuyapigia kura. Wakaketi, wakawa wanamchunga. Juu ya kichwa chake wakaweka shtaka dhidi yake lililoandikwa, “Huyu ni Yesu, Mfalme wa Wayahudi.” Wanyanganyi wawili walisulubiwa pia pamoja naye, mmoja upande wa kushoto na mwingine upande wa kulia. Watu waliokuwa wanapita mahali hapo walimtukana wakitikisa vichwa vyao na kusema, “Wewe! Si ulijidai kulivunja hekalu na kulijenga kwa siku tatu? Sasa jiokoe mwenyewe. Kama wewe ni Mwana wa Mungu, basi, shuka msalabani!” Hali kadhalika na makuhani wakuu pamoja na waalimu wa sheria na wazee walimdhihaki wakisema, “Aliwaokoa wengine, lakini kujiokoa mwenyewe hawezi! Ati yeye ni mfalme wa Wayahudi! Basi, sasa na ashuke msalabani, nasi tutamwamini. Alimtumainia Mungu na kusema ati yeye ni Mwana wa Mungu; basi, Mungu na amwokoe kama anamtaka.” Hali kadhalika na wale waliosulubiwa pamoja naye wakamtukana. Tangu saa sita mchana mpaka saa tisa, giza likaikumba nchi yote. Mnamo saa tisa Yesu akalia kwa sauti kubwa, “Eli, Eli, lema sabakthani?” Maana yake, “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?” Lakini wale waliosimama pale waliposikia hivyo wakasema, “Anamwita Elia.” Mmoja wao akakimbia, akachukua sifongo, akaichovya katika siki, akaiweka juu ya mwanzi, akampa anywe. Wengine wakasema, “Acha tuone kama Elia anakuja kumwokoa.” Basi, Yesu akalia tena kwa sauti kubwa, akakata roho. Hapo pazia la hekalu likapasuka vipande viwili, toka juu mpaka chini; nchi ikatetemeka; miamba ikapasuka; makaburi yakafunguka na watu wengi wa Mungu waliokufa wakafufuliwa; nao, baada ya kufufuka kwake, wakatoka makaburini, wakaingia katika mji mtakatifu, wakaonekana na watu wengi. Basi, jemadari na wale waliokuwa wakimlinda Yesu walipoona tetemeko la ardhi na yale mambo yaliyotukia, wakaogopa sana, wakasema, “Hakika mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu.” Mahali hapo walikuwapo wanawake wengi wakitazama kwa mbali. Hao ndio wale waliomfuata Yesu kutoka Galilaya wakimtumikia. Miongoni mwao walikuwa Maria Magdalene, Maria mama yao Yakobo na Yosefu, pamoja na mama yao wana wa Zebedayo. Ilipokuwa jioni, akaja mtu mmoja tajiri mwenyeji wa Arimathaya, jina lake Yosefu. Yeye pia alikuwa mwanafunzi wa Yesu. Akamwendea Pilato, akaomba apewe mwili wa Yesu. Basi, Pilato akaamuru apewe. Yosefu akauchukua ule mwili, akauzungushia sanda safi ya kitani, akauweka ndani ya kaburi lake jipya alilokuwa amelichonga katika mwamba. Kisha akavingirisha jiwe kubwa mbele ya mlango wa kaburi, akaenda zake. Maria Magdalene na yule Maria mwingine walikuwa wameketi kulielekea kaburi. Kesho yake, yaani siku iliyofuata ile ya Maandalio, makuhani wakuu na Mafarisayo walimwendea Pilato, Wakasema, “Mheshimiwa, tunakumbuka kwamba yule mdanganyifu alisema kabla ya kufa ati, ‘Baada ya siku tatu nitafufuka.’ Kwa hiyo amuru kaburi lilindwe mpaka siku ya tatu ili wanafunzi wake wasije wakamwiba na kuwaambia watu kwamba amefufuka. Uongo huu wa mwisho utakuwa mbaya zaidi kuliko ule wa awali.” Pilato akawaambia, “Haya, mnao walinzi; nendeni mkalinde kadiri mjuavyo.” Basi, wakaenda, wakalilinda kaburi, wakatia mhuri juu ya lile jiwe na kuacha hapo askari walinzi.