Mathayo 27:32-66
Mathayo 27:32-66 NENO
Walipokuwa wakienda, wakakutana na mtu mmoja kutoka Kirene, jina lake Simoni, nao wakamlazimisha kuubeba ule msalaba. Wakafika mahali palipoitwa Golgotha (maana yake ni Mahali pa Fuvu la Kichwa). Hapo wakampa Isa divai iliyochanganywa na nyongo ili anywe; lakini alipoionja, akakataa kuinywa. Walipokwisha kumsulubisha, wakagawana mavazi yake kwa kuyapigia kura. [Hili lilifanyika ili litimie neno lililonenwa na nabii, “Waligawa nguo zangu miongoni mwao na vazi langu wakalipigia kura.”] Kisha wakaketi, wakamchunga. Juu ya kichwa chake, kwenye msalaba, wakaandika shtaka lake hivi: HUYU NI ISA MFALME WA WAYAHUDI. Wanyang’anyi wawili walisulubiwa pamoja naye, mmoja upande wake wa kuume na mwingine upande wa kushoto. Watu waliokuwa wakipita njiani wakamtukana huku wakitikisa vichwa vyao, na kusema, “Wewe ambaye utalivunja Hekalu na kulijenga kwa siku tatu, jiokoe mwenyewe basi! Kama wewe ni Mwana wa Mungu, shuka msalabani.” Vivyo hivyo, viongozi wa makuhani, walimu wa Torati pamoja na wazee wakamdhihaki, wakisema, “Aliwaokoa wengine, lakini hawezi kujiokoa mwenyewe! Yeye ni mfalme wa Israeli! Ashuke sasa msalabani, nasi tutamwamini. Anamwamini Mungu, basi Mungu na amwokoe sasa kama anamtaka, kwa maana alisema, ‘Mimi ni Mwana wa Mungu.’ ” Hata wale wanyang’anyi waliosulubiwa pamoja naye wakamtukana vivyo hivyo. Tangu saa sita hadi saa tisa giza liliifunika nchi yote. Ilipofika saa tisa, Isa akapaza sauti akalia, “Eloi, Eloi, lama sabakthani?” (maana yake, “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?”) Baadhi ya watu waliokuwa wamesimama pale waliposikia hayo, wakasema, “Anamwita Ilya.” Ghafula mmoja wao akaenda mbio na kuleta sifongo, akaichovya kwenye siki, akaiweka kwenye mwanzi na akampa Isa ili anywe. Wengine wakasema, “Basi mwacheni. Hebu tuone kama Ilya atakuja kumwokoa.” Isa alipolia tena kwa sauti kuu, akaitoa roho yake. Wakati huo huo pazia la Hekalu likachanika vipande viwili, kuanzia juu hadi chini. Dunia ikatetemeka na miamba ikapasuka. Makaburi yakafunguka na miili ya watakatifu waliokuwa wamekufa ikafufuliwa. Wakatoka makaburini, na baada ya Isa kufufuka, waliingia kwenye Mji Mtakatifu na kuwatokea watu wengi. Basi yule jemadari na wale waliokuwa pamoja naye wakimlinda Isa walipoona lile tetemeko na yale yote yaliyokuwa yametukia, waliogopa sana, wakapaza sauti na kusema, “Hakika huyu alikuwa Mwana wa Mungu!” Wanawake wengi walikuwa pale wakitazama kwa mbali. Hawa walikuwa wamemfuata Isa tangu Galilaya ili kushughulikia mahitaji yake. Miongoni mwao walikuwemo Mariamu Magdalene, na Mariamu mama yao Yakobo na Yusufu, na mama yao wana wa Zebedayo. Ilipofika jioni, alifika mtu mmoja tajiri kutoka Arimathaya aitwaye Yusufu, ambaye pia alikuwa mwanafunzi wa Isa. Akamwendea Pilato ili kumwomba mwili wa Isa. Pilato akaamuru apewe. Yusufu akauchukua mwili wa Isa, akaufunga kwa kitambaa cha kitani safi, na kuuweka katika kaburi lake mwenyewe jipya, alilokuwa amelichonga kwenye mwamba. Kisha akavingirisha jiwe kubwa katika ingilio la kaburi, akaenda zake. Mariamu Magdalene na yule Mariamu mwingine walikuwa mahali pale, wakiwa wameketi mkabala na kaburi. Kesho yake, yaani siku iliyofuata ile ya Maandalizi ya Sabato, viongozi wa makuhani na Mafarisayo wakamwendea Pilato na kusema, “Bwana, tumekumbuka kwamba yule mdanganyifu wakati alikuwa bado hai alisema, ‘Baada ya siku tatu nitafufuka.’ Basi uamuru kaburi lilindwe kwa uthabiti hadi baada ya siku tatu. La sivyo, wanafunzi wake wanaweza kuja kuuiba mwili wake na kuwaambia watu kwamba amefufuliwa kutoka kwa wafu. Udanganyifu huu wa mwisho utakuwa mbaya kuliko ule wa kwanza.” Pilato akawaambia, “Ninyi mnao askari walinzi. Nendeni, liwekeeni ulinzi kadiri mnavyoweza.” Hivyo basi wakaenda na walinzi ili kulilinda kaburi kwa uthabiti, wakatia muhuri kwenye lile jiwe na kuweka ulinzi.