Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mathayo 26:47-56

Mathayo 26:47-56 BHN

Basi, Yesu alipokuwa bado anasema nao, mara akaja Yuda, mmoja wa wale kumi na wawili. Pamoja naye walikuja watu wengi wenye mapanga na marungu ambao walitumwa na makuhani wakuu na wazee wa watu. Huyo aliyetaka kumsaliti Yesu, alikuwa amekwisha kuwapa ishara akisema: “Yule nitakayembusu ndiye; mkamateni.” Basi, Yuda akamkaribia Yesu, akamwambia, “Shikamoo, Mwalimu!” Kisha akambusu. Yesu akamwambia, “Rafiki, fanya ulichokuja kufanya.” Hapo wale watu wakaja, wakamkamata Yesu, wakamtia nguvuni. Mmoja wa wale waliokuwa pamoja na Yesu akanyosha mkono, akauchomoa upanga wake, akampiga mtumishi wa kuhani mkuu, akamkata sikio. Hapo Yesu akamwambia, “Rudisha upanga wako alani, maana yeyote anayeutumia upanga, atakufa kwa upanga. Je, hamjui kwamba ningeweza kumwomba Baba yangu naye mara angeniletea zaidi ya vikosi kumi na viwili vya malaika? Lakini yatatimiaje Maandiko Matakatifu yasemayo kwamba ndivyo inavyopaswa kuwa?” Wakati huohuo Yesu akauambia huo umati wa watu waliokuja kumtia nguvuni, “Je, mmekuja kunikamata kwa mapanga na marungu kana kwamba mimi ni mnyanganyi? Kila siku nilikuwa hekaluni nikifundisha, na hamkunikamata! Lakini haya yote yametendeka ili maandiko ya manabii yatimie.” Kisha wanafunzi wote wakamwacha, wakakimbia.

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Mathayo 26:47-56