Mathayo 26:47-56
Mathayo 26:47-56 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, Yesu alipokuwa bado anasema nao, mara akaja Yuda, mmoja wa wale kumi na wawili. Pamoja naye walikuja watu wengi wenye mapanga na marungu ambao walitumwa na makuhani wakuu na wazee wa watu. Huyo aliyetaka kumsaliti Yesu, alikuwa amekwisha kuwapa ishara akisema: “Yule nitakayembusu ndiye; mkamateni.” Basi, Yuda akamkaribia Yesu, akamwambia, “Shikamoo, Mwalimu!” Kisha akambusu. Yesu akamwambia, “Rafiki, fanya ulichokuja kufanya.” Hapo wale watu wakaja, wakamkamata Yesu, wakamtia nguvuni. Mmoja wa wale waliokuwa pamoja na Yesu akanyosha mkono, akauchomoa upanga wake, akampiga mtumishi wa kuhani mkuu, akamkata sikio. Hapo Yesu akamwambia, “Rudisha upanga wako alani, maana yeyote anayeutumia upanga, atakufa kwa upanga. Je, hamjui kwamba ningeweza kumwomba Baba yangu naye mara angeniletea zaidi ya vikosi kumi na viwili vya malaika? Lakini yatatimiaje Maandiko Matakatifu yasemayo kwamba ndivyo inavyopaswa kuwa?” Wakati huohuo Yesu akauambia huo umati wa watu waliokuja kumtia nguvuni, “Je, mmekuja kunikamata kwa mapanga na marungu kana kwamba mimi ni mnyanganyi? Kila siku nilikuwa hekaluni nikifundisha, na hamkunikamata! Lakini haya yote yametendeka ili maandiko ya manabii yatimie.” Kisha wanafunzi wote wakamwacha, wakakimbia.
Mathayo 26:47-56 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi alipokuwa katika kusema, tazama, Yuda, mmoja wa wale Kumi na Wawili akaja, na pamoja naye kundi kubwa wenye panga na marungu, wametoka kwa wakuu wa makuhani na wazee wa watu. Na yule mwenye kumsaliti alikuwa amewapa ishara, akisema, Nitakayembusu, huyo ndiye; mkamateni. Mara akamwendea Yesu, akasema, Salamu, Rabi, akambusu. Yesu akamwambia, Rafiki, fanya ulilolijia. Wakaenda, wakanyosha mikono yao wakamkamata Yesu. Na tazama, mmoja wa wale waliokuwa pamoja na Yesu akanyosha mkono wake, akaufuta upanga wake, akampiga mtumwa wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio. Ndipo Yesu akamwambia, Rudisha upanga wako mahali pake, maana wote waushikao upanga, wataangamia kwa upanga. Ama wadhani ya kuwa mimi siwezi kumsihi Baba yangu, naye ataniletea sasa hivi zaidi ya majeshi kumi na mawili ya malaika? Yatatimizwaje basi maandiko, ya kwamba hivyo ndivyo vilivyopasa kujiri? Saa ile Yesu akawaambia makutano, Je, mmetoka kama kumkamata mnyang'anyi, wenye panga na marungu, ili kunishika? Kila siku niliketi hekaluni nikifundisha, msinikamate. Lakini haya yote yamekuwa, ili maandiko ya manabii yatimizwe. Ndipo wanafunzi wote wakamwacha, wakakimbia.
Mathayo 26:47-56 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi alipokuwa katika kusema, tazama, Yuda, mmoja wa wale Thenashara akaja, na pamoja naye kundi kubwa wenye panga na marungu, wametoka kwa wakuu wa makuhani na wazee wa watu. Na yule mwenye kumsaliti alikuwa amewapa ishara, akisema, Nitakayembusu, huyo ndiye; mkamateni. Mara akamwendea Yesu, akasema, Salamu, Rabi, akambusu. Yesu akamwambia, Rafiki, fanya ulilolijia. Wakaenda, wakanyosha mikono yao wakamkamata Yesu. Na tazama, mmoja wao waliokuwa pamoja na Yesu akanyosha mkono wake, akaufuta upanga wake, akampiga mtumwa wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio. Ndipo Yesu akamwambia, Rudisha upanga wako mahali pake, maana wote waushikao upanga, wataangamia kwa upanga. Ama wadhani ya kuwa mimi siwezi kumsihi Baba yangu, naye ataniletea sasa hivi zaidi ya majeshi kumi na mawili ya malaika? Yatatimizwaje basi maandiko, ya kwamba hivyo ndivyo vilivyopasa kujiri? Saa ile Yesu akawaambia makutano, Je, mmetoka kama kumkamata mnyang’anyi, wenye panga na marungu, ili kunishika? Kila siku naliketi hekaluni nikifundisha, msinikamate. Lakini haya yote yamekuwa, ili maandiko ya manabii yatimizwe. Ndipo wanafunzi wote wakamwacha, wakakimbia.
Mathayo 26:47-56 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Alipokuwa bado anazungumza, Yuda, mmoja wa wale Kumi na Wawili, akafika. Alikuwa amefuatana na umati mkubwa wa watu wenye panga na marungu, waliokuwa wametumwa na viongozi wa makuhani na wazee wa watu. Basi msaliti alikuwa amewapa hao watu ishara, kwamba: “Yule nitakayembusu ndiye. Mkamateni.” Mara Yuda akamjia Yesu na kumsalimu, “Salamu, Rabi!” Akambusu. Yesu akamwambia, “Rafiki, fanya kile ulichokuja kufanya hapa.” Kisha wale watu wakasogea mbele, wakamkamata Yesu. Ghafula mmoja wa wale waliokuwa na Yesu alipoona hivyo, akaushika upanga wake, akauchomoa na kumpiga mtumishi wa kuhani mkuu, akamkata sikio. Ndipo Yesu akamwambia, “Rudisha upanga wako mahali pake, kwa maana wote watumiao upanga watakufa kwa upanga. Je, unadhani siwezi kumwomba Baba yangu naye mara moja akaniletea zaidi ya majeshi kumi na mawili ya malaika? Lakini je, yale Maandiko yanayotabiri kwamba ni lazima itendeke hivi yatatimiaje?” Wakati huo, Yesu akawaambia ule umati wa watu, “Je, mmekuja na panga na marungu kunikamata kana kwamba mimi ni mnyangʼanyi? Siku kwa siku niliketi Hekaluni nikifundisha, mbona hamkunikamata? Lakini haya yote yametukia ili maandiko ya manabii yapate kutimia.” Ndipo wanafunzi wake wote wakamwacha na kukimbia.