Mathayo 24:36-51
Mathayo 24:36-51 BHN
“Lakini, juu ya siku au saa hiyo, hakuna mtu ajuaye itakuja lini; wala malaika wa mbinguni, wala Mwana; Baba peke yake ndiye ajuaye. Kwa maana kama ilivyokuwa nyakati za Noa, ndivyo itakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Mtu. Maana nyakati hizo, kabla ya gharika kuu, watu walikuwa wakila na kunywa, wakioa na kuolewa, mpaka Noa alipoingia ndani ya ile safina. Hawakujua kuna nini mpaka ile gharika ilipotokea, ikawakumba wote. Ndivyo itakavyokuwa wakati Mwana wa Mtu atakapokuja. Wakati huo watu wawili watakuwa shambani; mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa. Kina mama wawili watakuwa wanasaga nafaka, mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa. Basi, kesheni, kwa maana hamjui siku atakayokuja Bwana wenu. Lakini kumbukeni jambo hili: Kama mwenye nyumba angejua siku mwizi atakapofika, angekesha, wala hangeiacha nyumba yake ivunjwe. Kwa hiyo, nanyi pia muwe tayari, kwa maana Mwana wa Mtu atakuja saa msiyoitazamia.” Yesu akaendelea kusema, “Ni nani basi mtumishi mwaminifu na mwenye busara, ambaye bwana wake atamweka juu ya watu wake, awape chakula kwa wakati wake? Heri mtumishi yule ambaye bwana wake atakapokuja atamkuta akifanya hivyo. Kweli nawaambieni, atamweka mtumishi huyo aisimamie mali yake yote. Lakini kama mtumishi mbaya akijisemea moyoni: ‘Bwana wangu amekawia kurudi,’ kisha akaanza kuwapiga watumishi wenzake, akaanza kula na kunywa pamoja na walevi, bwana wake atakuja siku asiyoitazamia na saa asiyoijua. Atamwadhibu vibaya na kumweka kundi moja na wanafiki. Huko kutakuwa na kilio na kusaga meno.