Mathayo 24:36-51
Mathayo 24:36-51 SRUV
Lakini kuhusu siku ile na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni, wala Mwana, ila Baba peke yake. Kwa maana kama vile ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. Kwa kuwa kama vile siku zile zilizokuwa kabla ya Gharika watu walivyokuwa wakila, na kunywa, wakioa na kuolewa, hadi siku ile aliyoingia Nuhu katika safina, wasitambue, hata Gharika ikaja, ikawachukua wote, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. Wakati ule watu wawili watakuwako shambani; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa; wanawake wawili watakuwa wakisaga; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa. Kesheni basi; kwa maana hamjui ni siku ipi atakayokuja Bwana wenu. Lakini fahamuni neno hili; kama mwenye nyumba angaliujua ule wakati mwizi atakaokuja, angalikesha, wala asingaliiacha nyumba yake kuvunjwa. Kwa sababu hiyo ninyi nanyi jiwekeni tayari; kwa kuwa katika saa msiyotazamia Mwana wa Adamu yuaja. Ni nani basi yule mtumwa mwaminifu mwenye akili, ambaye bwana wake alimweka juu ya nyumba yake, awape watu chakula kwa wakati wake? Heri mtumwa yule, ambaye bwana wake ajapo atamkuta akifanya hivyo. Amin, nawaambieni, atamweka juu ya vitu vyake vyote. Lakini mtumwa yule mbaya akisema moyoni mwake, Bwana wangu anakawia; akaanza kuwapiga watumwa wenzake, na kula na kunywa pamoja na walevi; bwana wake mtumwa huyo atakuja siku asiyotazamia, na saa asiyojua, atamkata vipande viwili, na kumwekea fungu lake pamoja na wanafiki; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.