Mathayo 21:12-17
Mathayo 21:12-17 BHN
Basi, Yesu akaingia hekaluni, akawafukuza nje watu waliokuwa wanauza na kununua vitu ndani ya hekalu; akazipindua meza za wale waliokuwa wanavunja fedha, na viti vya wale waliokuwa wanauza njiwa. Akawaambia, “Imeandikwa katika Maandiko Matakatifu: ‘Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala.’ Lakini nyinyi mmeifanya kuwa pango la wanyanganyi.” Vipofu na vilema wengine walimwendea huko hekaluni, naye Yesu akawaponya. Basi, makuhani wakuu na waalimu wa sheria walipoyaona maajabu aliyoyafanya Yesu, na pia watoto walipokuwa wanapaza sauti zao hekaluni wakisema: “Sifa kwa Mwana wa Daudi,” wakakasirika. Hivyo wakamwambia, “Je, husikii wanachosema?” Yesu akawajibu, “Naam, nasikia! Je hamjapata kusoma Maandiko haya? ‘Kwa vinywa vya watoto wadogo na wachanga wajipatia sifa kamili.’” Basi, akawaacha, akatoka nje ya mji na kwenda Bethania, akalala huko.