Mt 21:12-17
Mt 21:12-17 SUV
Yesu akaingia ndani ya hekalu, akawafukuza wote waliokuwa wakiuza na kununua hekaluni, akazipindua meza za wabadili fedha, na viti vyao waliokuwa wakiuza njiwa; akawaambia, Imeandikwa, Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala; bali ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang’anyi. Na vipofu na viwete wakamwendea mle hekaluni, akawaponya. Lakini wakuu wa makuhani na waandishi walipoyaona maajabu aliyoyafanya, na watoto waliopaza sauti zao hekaluni, wakisema, Hosana, Mwana wa Daudi! Walikasirika, wakamwambia, Wasikia hawa wasemavyo? Yesu akawaambia, Naam; hamkupata kusoma, Kwa vinywa vya watoto wachanga na wanyonyao umekamilisha sifa? Akawaacha, akatoka nje ya mji mpaka Bethania, akalala huko.