Mathayo 15:21-39
Mathayo 15:21-39 BHN
Yesu aliondoka mahali hapo akaenda kukaa katika sehemu za Tiro na Sidoni. Basi, mama mmoja Mkanaani wa nchi hiyo alimjia, akapaza sauti: “Bwana, Mwana wa Daudi, nionee huruma! Binti yangu anasumbuliwa na pepo.” Lakini Yesu hakumjibu neno. Basi, wanafunzi wake wakamwendea, wakamwambia, “Mwambie aende zake kwa maana anatufuatafuata akipiga kelele.” Yesu akajibu, “Sikutumwa ila kwa watu wa Israeli waliopotea kama kondoo.” Hapo huyo mama akaja, akamsujudia, akasema, “Bwana, nisaidie.” Yesu akamjibu, “Si vizuri kuchukua chakula cha watoto na kuwatupia mbwa.” Huyo mama akajibu, “Ni kweli, Bwana; lakini hata mbwa hula makombo yanayoanguka kutoka meza ya bwana wao.” Hapo Yesu akamjibu, “Mama, imani yako ni kubwa; basi, ufanyiwe kama unavyotaka.” Yule binti yake akapona wakati huohuo. Yesu alitoka hapo akaenda kando ya ziwa Galilaya, akapanda mlimani, akaketi. Watu wengi sana wakamjia wakiwaleta vilema, vipofu, viwete, bubu na wengine wengi waliokuwa wagonjwa, wakawaweka mbele ya miguu yake, naye Yesu akawaponya. Umati ule wa watu ulishangaa sana ulipoona bubu wakiongea, waliokuwa wamelemaa wamepona, viwete wakitembea na vipofu wakiona; watu wakamsifu Mungu wa Israeli. Basi, Yesu aliwaita wanafunzi wake, akasema, “Nawaonea huruma watu hawa kwa sababu wamekuwa nami kwa siku tatu, wala hawana chakula. Sipendi kuwaacha waende zao bila kula, wasije wakazimia njiani.” Wanafunzi wakamwambia, “Hapa tuko nyikani; tutapata wapi chakula cha kuwatosha watu wengi hivi?” Yesu akawauliza, “Mnayo mikate mingapi?” Wakamjibu, “Saba na visamaki vichache.” Basi, Yesu akawaamuru watu wakae chini. Akaitwaa ile mikate saba na vile visamaki, akamshukuru Mungu, akavimega, akawapa wanafunzi, nao wakawagawia watu. Wote wakala, wakashiba. Kisha wakakusanya mabaki, wakajaza vikapu saba. Hao waliokula walikuwa wanaume 4,000, bila kuhesabu wanawake na watoto. Basi, Yesu akawaaga watu, akapanda mashua, akaenda katika eneo la Magadani.