Mathayo 15:21-39
Mathayo 15:21-39 Biblia Habari Njema (BHN)
Yesu aliondoka mahali hapo akaenda kukaa katika sehemu za Tiro na Sidoni. Basi, mama mmoja Mkanaani wa nchi hiyo alimjia, akapaza sauti: “Bwana, Mwana wa Daudi, nionee huruma! Binti yangu anasumbuliwa na pepo.” Lakini Yesu hakumjibu neno. Basi, wanafunzi wake wakamwendea, wakamwambia, “Mwambie aende zake kwa maana anatufuatafuata akipiga kelele.” Yesu akajibu, “Sikutumwa ila kwa watu wa Israeli waliopotea kama kondoo.” Hapo huyo mama akaja, akamsujudia, akasema, “Bwana, nisaidie.” Yesu akamjibu, “Si vizuri kuchukua chakula cha watoto na kuwatupia mbwa.” Huyo mama akajibu, “Ni kweli, Bwana; lakini hata mbwa hula makombo yanayoanguka kutoka meza ya bwana wao.” Hapo Yesu akamjibu, “Mama, imani yako ni kubwa; basi, ufanyiwe kama unavyotaka.” Yule binti yake akapona wakati huohuo. Yesu alitoka hapo akaenda kando ya ziwa Galilaya, akapanda mlimani, akaketi. Watu wengi sana wakamjia wakiwaleta vilema, vipofu, viwete, bubu na wengine wengi waliokuwa wagonjwa, wakawaweka mbele ya miguu yake, naye Yesu akawaponya. Umati ule wa watu ulishangaa sana ulipoona bubu wakiongea, waliokuwa wamelemaa wamepona, viwete wakitembea na vipofu wakiona; watu wakamsifu Mungu wa Israeli. Basi, Yesu aliwaita wanafunzi wake, akasema, “Nawaonea huruma watu hawa kwa sababu wamekuwa nami kwa siku tatu, wala hawana chakula. Sipendi kuwaacha waende zao bila kula, wasije wakazimia njiani.” Wanafunzi wakamwambia, “Hapa tuko nyikani; tutapata wapi chakula cha kuwatosha watu wengi hivi?” Yesu akawauliza, “Mnayo mikate mingapi?” Wakamjibu, “Saba na visamaki vichache.” Basi, Yesu akawaamuru watu wakae chini. Akaitwaa ile mikate saba na vile visamaki, akamshukuru Mungu, akavimega, akawapa wanafunzi, nao wakawagawia watu. Wote wakala, wakashiba. Kisha wakakusanya mabaki, wakajaza vikapu saba. Hao waliokula walikuwa wanaume 4,000, bila kuhesabu wanawake na watoto. Basi, Yesu akawaaga watu, akapanda mashua, akaenda katika eneo la Magadani.
Mathayo 15:21-39 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Yesu akaondoka huko, akaenda kando pande za Tiro na Sidoni. Na tazama, mwanamke Mkanaani wa mipaka ile akatokea, akampazia sauti akisema, Unirehemu, Bwana, Mwana wa Daudi; binti yangu amepagawa sana na pepo. Wala yeye hakumjibu neno. Nao wanafunzi wake wakamwendea, wakamwomba, wakisema, Mwache aende zake; kwa kuwa anaendelea kutupigia makelele nyuma yetu. Akajibu, akasema, Sikutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli. Naye akaja akamsujudia, akisema Bwana, unisaidie. Akajibu, akasema, Si vema kukitwaa chakula cha watoto na kuwatupia mbwa. Akasema, Ndiyo, Bwana, lakini hata mbwa hula makombo yaangukayo mezani pa bwana zao. Ndipo Yesu akajibu, akamwambia, Mama, imani yako ni kubwa; na iwe kwako kama utakavyo. Akapona binti yake tangu saa ile. Yesu akaondoka huko, akafika kando ya bahari ya Galilaya; akapanda mlimani, akaketi huko. Wakamwendea makutano mengi wakimletea viwete, vipofu, mabubu, vilema, na wengine wengi, wakawaweka miguuni pake; akawaponya; hata ule mkutano wakastaajabu, walipowaona mabubu wanasema, vilema wanakuwa wazima, viwete wanakwenda, na vipofu wanaona; wakamtukuza Mungu wa Israeli. Yesu akawaita wanafunzi wake, akasema, Nawahurumia mkutano, kwa kuwa yapata siku tatu wamekaa pamoja nami, wala hawana kitu cha kula, tena sitaki kuwaaga wakiwa na njaa, wasije wakazimia njiani. Wanafunzi wake wakamwambia, Tupate wapi mikate mingi hapa nyikani, hata kushibisha mkutano mkuu namna hii? Yesu akawaambia, Mnayo mikate mingapi? Wakasema, Saba, na visamaki vichache. Akawaagiza mkutano waketi chini; akaitwaa ile mikate saba na vile visamaki, akashukuru akavimega, akawapa wanafunzi wake, nao wanafunzi wakawapa makutano. Wakala wote wakashiba; wakayaokota mabaki ya vipande vya mikate makanda saba, yamejaa. Nao waliokula walikuwa wanaume elfu nne, bila kuhesabu wanawake na watoto. Akawaaga makutano, akapanda katika mashua, akaenda pande za Magadani.
Mathayo 15:21-39 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Yesu akaondoka huko, akaenda kando pande za Tiro na Sidoni. Na tazama, mwanamke Mkananayo wa mipaka ile akatokea, akampazia sauti akisema, Unirehemu, Bwana, Mwana wa Daudi; binti yangu amepagawa sana na pepo. Wala yeye hakumjibu neno. Nao wanafunzi wake wakamwendea, wakamwomba, wakisema, Mwache aende zake; kwa maana anapiga kelele nyuma yetu. Akajibu, akasema, Sikutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli. Naye akaja akamsujudia, akisema Bwana, unisaidie. Akajibu, akasema, Si vema kukitwaa chakula cha watoto na kuwatupia mbwa. Akasema, Ndiyo, Bwana, lakini hata mbwa hula makombo yaangukayo mezani pa bwana zao. Ndipo Yesu akajibu, akamwambia, Mama, imani yako ni kubwa; na iwe kwako kama utakavyo. Akapona binti yake tangu saa ile. Yesu akaondoka huko, akafika kando ya bahari ya Galilaya; akapanda mlimani, akaketi huko. Wakamwendea makutano mengi wakimletea viwete, vipofu, mabubu, vilema, na wengine wengi, wakawaweka miguuni pake; akawaponya; hata ule mkutano wakastaajabu, walipowaona mabubu wanasema, vilema wanakuwa wazima, viwete wanakwenda, na vipofu wanaona; wakamtukuza Mungu wa Israeli. Yesu akawaita wanafunzi wake, akasema, Nawahurumia mkutano, kwa kuwa yapata siku tatu wamekaa pamoja nami, wala hawana kitu cha kula, tena kuwaaga wakifunga sipendi, wasije wakazimia njiani. Wanafunzi wake wakamwambia, Tupate wapi mikate mingi hapa nyikani, hata kushibisha mkutano mkuu namna hii? Yesu akawaambia, Mnayo mikate mingapi? Wakasema, Saba, na visamaki vichache. Akawaagiza mkutano waketi chini; akaitwaa ile mikate saba na vile visamaki, akashukuru akavimega, akawapa wanafunzi wake, nao wanafunzi wakawapa makutano. Wakala wote wakashiba; wakayaokota masazo ya vipande vya mikate makanda saba, yamejaa. Nao waliokula walikuwa wanaume elfu nne, bila wanawake na watoto. Akawaaga makutano, akapanda chomboni, akaenda pande za Magadani.
Mathayo 15:21-39 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Isa aliondoka mahali pale, akaenda sehemu za Tiro na Sidoni. Mwanamke mmoja Mkanaani aliyeishi sehemu jirani na hizo akaja kwake akilia, akasema, “Nihurumie, Ee Bwana, Mwana wa Daudi! Binti yangu amepagawa na pepo mchafu, na anateseka sana.” Lakini Isa hakumjibu neno. Hivyo wanafunzi wake wakamwendea na kumsihi sana, wakisema, “Mwambie aende zake, kwa maana anaendelea kutupigia kelele.” Isa akajibu, “Nimetumwa tu kwa ajili ya kondoo wa Israeli waliopotea.” Lakini yule mwanamke akaja, akapiga magoti mbele ya Isa, akasema, “Bwana, nisaidie!” Isa akajibu, “Si haki kuchukua chakula cha watoto na kuwatupia mbwa.” Yule mwanamke akajibu, “Ndiyo, Bwana, lakini hata mbwa hula makombo yanayoanguka kutoka kwa meza za bwana zao.” Ndipo Isa akamwambia, “Mwanamke, imani yako ni kubwa! Iwe kwako kama unavyotaka.” Naye binti yake akapona tangu saa ile. Isa akaondoka na kwenda kando ya Bahari ya Galilaya. Kisha akapanda mlimani, akaketi huko. Umati mkubwa wa watu wakamjia, wakiwaleta vilema, vipofu, viwete, bubu na wengine wengi, wakawaweka miguuni pake; naye akawaponya. Hao watu wakashangaa walipoona bubu wakisema, vilema wakipona, viwete wakitembea na vipofu wakiona, wakamtukuza Mungu wa Israeli. Kisha Isa akawaita wanafunzi wake, akawaambia, “Ninahurumia umati huu wa watu, kwa sababu sasa wamekuwa pamoja nami kwa muda wa siku tatu, na hawana chakula chochote. Nami sipendi kuwaaga watu wakiwa na njaa, wasije wakazimia njiani.” Wanafunzi wake wakasema, “Tutapata wapi mikate ya kutosha kulisha umati mkubwa namna hii, nasi tuko nyikani?” Isa akawauliza, “Mnayo mikate mingapi?” Wakamjibu, “Tunayo mikate saba na visamaki vichache.” Isa akaagiza watu wote waketi chini. Kisha akachukua ile mikate saba na wale samaki, naye akamshukuru Mungu, akavimega na kuwapa wanafunzi wake, nao wakawapa watu. Wote wakala na kushiba. Baadaye wanafunzi wakakusanya vipande vilivyosalia, wakajaza vikapu saba. Idadi ya watu walikuwa wanaume elfu nne, bila kuhesabu wanawake na watoto. Baada ya kuaga umati wa watu, Isa aliingia katika mashua, akaenda sehemu za Magadani.