Malaki 1:6-14
Malaki 1:6-14 BHN
Mwenyezi-Mungu wa majeshi anawaambia hivi nyinyi makuhani mnaolidharau jina lake: “Mtoto humheshimu mzazi wake, na mtumishi humheshimu bwana wake. Ikiwa mimi ndiye Baba yenu, mbona mwanivunjia heshima? Ikiwa mimi ni bwana wenu, mbona hamniheshimu? Nanyi mnauliza, ‘Sisi tumekudharauje?’ Mwanidharau kwa kunitolea madhabahuni pangu tambiko ya chakula najisi. Lakini nyinyi mnauliza, ‘Tumekitiaje najisi?’ Mnakitia najisi kwa kuidharau madhabahu yangu. Mnaponitolea tambiko ya mnyama kipofu, au kilema, au mgonjwa, je, huo si uovu? Je, mtawala atapendezwa au kukufanyia hisani ukimpa zawadi ya mnyama kama huyo?” Kwa hiyo sasa enyi makuhani, mwombeni Mungu ili atuhurumie. Ikiwa mnamtolea matoleo ya aina hiyo, je, kweli atakuwa radhi nanyi? Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema, “Laiti angepatikana mtu mmoja miongoni mwenu ambaye angefunga milango ya hekalu ili msiwashe moto usiokubalika kwenye madhabahu yangu! Sipendezwi nanyi na sitaikubali tambiko yoyote mnayonitolea. Watu wa mataifa kote duniani, toka mawio ya jua hadi machweo yake, wanalitukuza jina langu. Kila mahali wananifukizia ubani na kunitolea tambiko zinazokubalika; maana jina langu linatukuzwa miongoni mwao. Lakini nyinyi mnalibeza jina langu pale mnapoichafua madhabahu yangu, na chakula mnachotoa juu yake mnakidharau. Mnasema, ‘Mambo haya yametuchosha mno,’ na mnanidharau. Mnaniletea tambiko za wanyama mliowapata kwa unyang'anyi, au walio vilema au wagonjwa. Je, nipokee tambiko hizo mikononi mwenu? Mimi Mwenyezi-Mungu nauliza. Na alaaniwe mtu yeyote anidanganyaye, ambaye huahidi kwa kiapo kunitolea tambiko mnyama safi kutoka katika kundi lake, lakini hunitolea tambiko mnyama mwenye kilema. Tazama, mimi ni mfalme mkuu, na watu wa mataifa yote hunicha.”