Luka 8:4-15
Luka 8:4-15 BHN
Wakati mmoja kundi kubwa la watu lilikuwa linakusanyika, na watu walikuwa wanamjia Yesu kutoka kila mji. Naye akawaambia mfano huu: “Mpanzi alikwenda kupanda mbegu zake. Alipokuwa akipanda hizo mbegu, nyingine zilianguka njiani, na wapita njia wakazikanyaga na ndege wakazila. Nyingine zilianguka penye mawe, na baada ya kuota zikanyauka kwa kukosa maji. Nyingine zilianguka kati ya miti ya miiba. Ile miti ya miiba ilipoota ikazisonga. Nyingine zilianguka katika udongo mzuri, zikaota na kuzaa asilimia mia.” Baada ya kusema hayo, akapaza sauti, akasema, “Mwenye masikio na asikie!” Wanafunzi wake Yesu wakamwuliza maana ya mfano huo. Naye akajibu, “Nyinyi mmejaliwa kujua siri za ufalme wa Mungu, lakini hao wengine sivyo; ila hao huambiwa kwa mifano, ili wakitazama wasiweze kuona, na wakisikia wasifahamu. “Basi, maana ya mfano huu ni hii: Mbegu ni neno la Mungu. Zile zilizoanguka njiani zinaonesha watu wale wanaosikia lile neno, halafu Ibilisi akaja na kuliondoa mioyoni mwao wasije wakaamini wakaokoka. Zile zilizoanguka penye mawe zinaonesha watu wale ambao wanaposikia juu ya lile neno hulipokea kwa furaha. Lakini kama zile mbegu, watu hao hawana mizizi maana husadiki kwa kitambo tu, na wanapojaribiwa hukata tamaa. Zile zilizoanguka kwenye miti ya miiba ni watu wale wanaosikia lile neno, lakini muda si muda, wanapokwenda zao, husongwa na wasiwasi, mali na anasa za maisha, nao hawazai matunda yakakomaa. Na zile zilizoanguka kwenye udongo mzuri ndio watu wale wanaolisikia lile neno, wakalizingatia kwa moyo mwema na wa utii. Hao huvumilia mpaka wakazaa matunda.