Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Luka 8:4-15

Luka 8:4-15 NEN

Umati mkubwa wa watu ulipokuwa ukija kwa Yesu kutoka kila mji, akawaambia mfano huu: “Mpanzi alitoka kwenda kupanda mbegu zake. Alipokuwa akitawanya mbegu, nyingine zilianguka kando ya njia; zikakanyagwa, nao ndege wa angani wakazila. Mbegu nyingine zilianguka penye miamba, nazo zilipoota, hiyo mimea ikakauka kwa kukosa unyevu. Nazo mbegu nyingine zilianguka kwenye miiba, nayo ile miiba ikakua pamoja nazo, na kuisonga hiyo mimea. Mbegu nyingine zilianguka kwenye udongo mzuri. Zikaota na kuzaa mara mia moja zaidi ya mbegu alizopanda.” Baada ya kusema haya, Yesu akapaza sauti, akasema, “Mwenye masikio ya kusikia, na asikie.” Wanafunzi wake wakamuuliza maana ya mfano huo. Naye akasema, “Ninyi mmepewa kufahamu siri za Ufalme wa Mungu, lakini kwa wengine nazungumza kwa mifano, ili, “ ‘ingawa wanatazama, wasione; ingawa wanasikiliza, wasielewe.’ “Maana ya mfano huu ni hii: Mbegu ni neno la Mungu. Zile zilizoanguka kando ya njia ni wale ambao husikia neno, naye ibilisi anakuja na kuliondoa neno kutoka mioyoni mwao, ili wasije wakaamini na kuokoka. Zile mbegu zilizoanguka kwenye mwamba ni wale ambao hulipokea neno kwa furaha wanapolisikia, lakini hawana mizizi. Wanaamini kwa muda mfupi, lakini wakati wa kujaribiwa huiacha imani. Zile mbegu zilizoanguka kwenye miiba ni mfano wa wale wanaosikia, lakini wanapoendelea husongwa na masumbufu ya maisha haya, utajiri na anasa, nao hawakui. Lakini zile mbegu zilizoanguka kwenye udongo mzuri ni mfano wa wale ambao hulisikia neno la Mungu na kulishika kwa moyo mnyofu wa utiifu, nao kwa kuvumilia kwingi huzaa matunda.

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Luka 8:4-15