Luka 22:24-38
Luka 22:24-38 BHN
Kulitokea ubishi kati ya hao mitume kuhusu nani miongoni mwao anayefikiriwa kuwa mkuu kuliko wengine. Yesu akawaambia, “Wafalme wa mataifa huwatawala watu wao kwa mabavu, nao huitwa wafadhili wa watu. Lakini isiwe hivyo kati yenu; bali, yule aliye mkuu kati yenu ni lazima awe mdogo wa wote, na aliye kiongozi lazima awe kama mtumishi. Kwa maana, ni nani aliye mkuu: Yule anayeketi mezani kula chakula, ama yule anayetumikia? Bila shaka ni yule anayeketi mezani kula chakula! Hata hivyo, mimi niko hapa kati yenu kama mtumishi. “Nyinyi ndio mliobaki nami wakati wote wa majaribu yangu; na, kama vile Baba yangu alivyonikabidhi ufalme, vivyo hivyo nami ninawakabidhi nyinyi ufalme. Mtakula na kunywa mezani pangu katika ufalme wangu na kuketi katika viti vya enzi kuyahukumu makabila kumi na mawili ya Israeli. “Simoni, Simoni! Sikiliza! Shetani alitaka kuwapepeta nyinyi kama mtu anavyopepeta ngano. Lakini mimi nimekuombea ili imani yako isipungue. Nawe utakaponirudia, watie moyo ndugu zako.” Naye Petro akamjibu, “Bwana, mimi niko tayari kwenda pamoja nawe gerezani, na hata kufa.” Yesu akamjibu, “Nakuambia wewe Petro, kabla jogoo hajawika leo utakuwa umenikana mara tatu.” Kisha, Yesu akawauliza wanafunzi wake, “Wakati nilipowatuma bila mfuko wa fedha wala mkoba wala viatu, mlitindikiwa chochote?” Wakajibu, “La.” Naye akawaambia, “Lakini sasa, yule aliye na mfuko wa fedha auchukue; na aliye na mkoba, hali kadhalika. Na yeyote asiye na upanga, auze koti lake anunue mmoja. Maana nawaambieni, haya maneno ya Maandiko Matakatifu: ‘Aliwekwa kundi moja na wahalifu,’ ni lazima yatimie. Naam, yale yanayonihusu yanafikia ukamilifu wake.” Nao wakasema, “Bwana, tazama; hapa kuna panga mbili.” Naye akasema, “Basi!”