Luka 22:24-38
Luka 22:24-38 Biblia Habari Njema (BHN)
Kulitokea ubishi kati ya hao mitume kuhusu nani miongoni mwao anayefikiriwa kuwa mkuu kuliko wengine. Yesu akawaambia, “Wafalme wa mataifa huwatawala watu wao kwa mabavu, nao huitwa wafadhili wa watu. Lakini isiwe hivyo kati yenu; bali, yule aliye mkuu kati yenu ni lazima awe mdogo wa wote, na aliye kiongozi lazima awe kama mtumishi. Kwa maana, ni nani aliye mkuu: Yule anayeketi mezani kula chakula, ama yule anayetumikia? Bila shaka ni yule anayeketi mezani kula chakula! Hata hivyo, mimi niko hapa kati yenu kama mtumishi. “Nyinyi ndio mliobaki nami wakati wote wa majaribu yangu; na, kama vile Baba yangu alivyonikabidhi ufalme, vivyo hivyo nami ninawakabidhi nyinyi ufalme. Mtakula na kunywa mezani pangu katika ufalme wangu na kuketi katika viti vya enzi kuyahukumu makabila kumi na mawili ya Israeli. “Simoni, Simoni! Sikiliza! Shetani alitaka kuwapepeta nyinyi kama mtu anavyopepeta ngano. Lakini mimi nimekuombea ili imani yako isipungue. Nawe utakaponirudia, watie moyo ndugu zako.” Naye Petro akamjibu, “Bwana, mimi niko tayari kwenda pamoja nawe gerezani, na hata kufa.” Yesu akamjibu, “Nakuambia wewe Petro, kabla jogoo hajawika leo utakuwa umenikana mara tatu.” Kisha, Yesu akawauliza wanafunzi wake, “Wakati nilipowatuma bila mfuko wa fedha wala mkoba wala viatu, mlitindikiwa chochote?” Wakajibu, “La.” Naye akawaambia, “Lakini sasa, yule aliye na mfuko wa fedha auchukue; na aliye na mkoba, hali kadhalika. Na yeyote asiye na upanga, auze koti lake anunue mmoja. Maana nawaambieni, haya maneno ya Maandiko Matakatifu: ‘Aliwekwa kundi moja na wahalifu,’ ni lazima yatimie. Naam, yale yanayonihusu yanafikia ukamilifu wake.” Nao wakasema, “Bwana, tazama; hapa kuna panga mbili.” Naye akasema, “Basi!”
Luka 22:24-38 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Yakatokea mashindano kati yao, kwamba ni nani anayehesabiwa kuwa mkubwa. Akawaambia, Wafalme wa Mataifa huwatawala, na wenye mamlaka juu yao huitwa Wenye fadhili; lakini kwenu ninyi sivyo; bali aliye mkubwa kwenu na awe kama aliye mdogo; na mwenye kuongoza kama yule atumikaye. Maana aliye mkubwa ni yupi? Yeye aketiye chakulani, au yule atumikaye? Siye yule aketiye chakulani? Lakini mimi kati yenu ni kama atumikaye. Nanyi ndinyi mliodumu pamoja nami katika majaribu yangu. Nami nawawekea ninyi ufalme, kama vile Baba yangu alivyoniwekea mimi; mpate kula na kunywa mezani pangu katika ufalme wangu; na kuketi katika viti vya enzi, huku mkiyahukumu makabila kumi na mawili ya Israeli. Akasema, Simoni, Simoni, tazama, Shetani amewataka ninyi apate kuwapepeta kama vile ngano; lakini nimekuombea wewe ili imani yako isipungue; nawe utakapoongoka waimarishe ndugu zako. Akamwambia, Bwana, niwapo pamoja nawe, mimi ni tayari kwenda gerezani au hata kifoni. Akasema, Nakuambia, Petro, jogoo hatawika leo, kabla wewe hujanikana mara tatu ya kuwa hunijui. Akawauliza, Je! Hapo nilipowatuma hamna mfuko, wala mkoba, wala viatu, mlipungukiwa na kitu? Wakasema, La! Akawaambia, Lakini sasa mwenye mfuko na auchukue, na mkoba vivyo hivyo; naye asiye na upanga, na auze joho lake akanunue. Kwa kuwa nawaambia, hayo yaliyoandikwa hayana budi kutimizwa kwangu; ya kuwa, Alihesabiwa pamoja na wahalifu. Kwa sababu yanipasayo yanao mwisho wake. Wakasema, Bwana, tazama, hapa pana panga mbili. Akawaambia, Basi.
Luka 22:24-38 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Yakatokea mashindano kati yao, kwamba ni nani anayehesabiwa kuwa mkubwa. Akawaambia, Wafalme wa Mataifa huwatawala, na wenye mamlaka juu yao huitwa Wenye fadhili; lakini kwenu ninyi sivyo; bali aliye mkubwa kwenu na awe kama aliye mdogo; na mwenye kuongoza kama yule atumikaye. Maana aliye mkubwa ni yupi? Yeye aketiye chakulani, au yule atumikaye? Siye yule aketiye chakulani? Lakini mimi kati yenu ni kama atumikaye. Nanyi ndinyi mliodumu pamoja nami katika majaribu yangu. Nami nawawekea ninyi ufalme, kama vile Baba yangu alivyoniwekea mimi; mpate kula na kunywa mezani pangu katika ufalme wangu; na kuketi katika viti vya enzi, huku mkiwahukumu kabila kumi na mbili za Israeli. Akasema, Simoni, Simoni, tazama, Shetani amewataka ninyi apate kuwapepeta kama vile ngano; lakini nimekuombea wewe ili imani yako isitindike; nawe utakapoongoka waimarishe ndugu zako. Akamwambia, Bwana, niwapo pamoja nawe, mimi ni tayari kwenda gerezani au hata kifoni. Akasema, Nakuambia, Petro, jogoo hatawika leo, kabla wewe hujanikana mara tatu ya kuwa hunijui. Akawauliza, Je! Hapo nilipowatuma hamna mfuko, wala mkoba, wala viatu, mlipungukiwa na kitu? Wakasema, La! Akawaambia, Lakini sasa mwenye mfuko na auchukue, na mkoba vivyo hivyo; naye asiye na upanga, na auze joho yake akanunue. Kwa kuwa nawaambia, hayo yaliyoandikwa hayana budi kutimizwa kwangu; ya kuwa, Alihesabiwa pamoja na wahalifu. Kwa sababu yanipasayo yanao mwisho wake. Wakasema, Bwana, tazama, hapa pana panga mbili. Akawaambia, Basi.
Luka 22:24-38 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Pia yakazuka mabishano katikati ya wanafunzi kwamba ni nani aliyeonekana kuwa mkuu kuliko wote miongoni mwao. Yesu akawaambia, “Wafalme na watu wa Mataifa huwatawala watu kwa nguvu. Nao wenye mamlaka juu yao hujiita ‘Wafadhili.’ Lakini ninyi msifanane nao. Bali yeye aliye mkuu kuliko wote miongoni mwenu, inampasa kuwa kama yeye aliye mdogo wa wote, naye atawalaye na awe kama yeye ahudumuye. Kwani ni nani aliye mkuu? Ni yule aketiye mezani au ni yule ahudumuye? Si ni yule aliyekaa mezani? Lakini mimi niko miongoni mwenu kama yule ahudumuye. Ninyi mmekuwa pamoja nami katika majaribu yangu. Nami kama Baba yangu alivyonipa ufalme, kadhalika mimi nami ninawapa ninyi, ili mpate kula na kunywa mezani pangu katika karamu ya ufalme wangu, na kukaa katika viti vya enzi, mkihukumu makabila kumi na mawili ya Israeli.” Yesu akasema, “Simoni, Simoni, sikiliza, Shetani ameomba kuwapepeta ninyi wote kama ngano. Lakini nimekuombea wewe Simoni ili imani yako isishindwe, nawe ukiisha kunirudia, uwaimarishe ndugu zako.” Petro akajibu, “Bwana, niko tayari kwenda pamoja nawe gerezani na hata kifoni.” Yesu akamjibu, “Ninakuambia Petro, kabla jogoo hajawika usiku wa leo, utakana mara tatu kwamba hunijui mimi.” Kisha Yesu akawauliza, “Nilipowatuma bila mfuko, wala mkoba, wala viatu, mlipungukiwa na kitu chochote?” Wakajibu, “La, hatukupungukiwa na kitu chochote.” Akawaambia, “Lakini sasa, aliye na mfuko na auchukue, na aliye na mkoba vivyo hivyo. Naye asiye na upanga, auze joho lake anunue mmoja. Kwa sababu, nawaambia, andiko hili lazima litimizwe juu yangu, kwamba, ‘Alihesabiwa pamoja na wakosaji’; kwa kweli yaliyoandikwa kunihusu mimi hayana budi kutimizwa.” Wanafunzi wake wakamwambia, “Bwana, tazama hapa kuna panga mbili.” Akawajibu, “Inatosha.”