Luka 22:24-38
Luka 22:24-38 NEN
Pia yakazuka mabishano katikati ya wanafunzi kwamba ni nani aliyeonekana kuwa mkuu kuliko wote miongoni mwao. Yesu akawaambia, “Wafalme na watu wa Mataifa huwatawala watu kwa nguvu. Nao wenye mamlaka juu yao hujiita ‘Wafadhili.’ Lakini ninyi msifanane nao. Bali yeye aliye mkuu kuliko wote miongoni mwenu, inampasa kuwa kama yeye aliye mdogo wa wote, naye atawalaye na awe kama yeye ahudumuye. Kwani ni nani aliye mkuu? Ni yule aketiye mezani au ni yule ahudumuye? Si ni yule aliyekaa mezani? Lakini mimi niko miongoni mwenu kama yule ahudumuye. Ninyi mmekuwa pamoja nami katika majaribu yangu. Nami kama Baba yangu alivyonipa ufalme, kadhalika mimi nami ninawapa ninyi, ili mpate kula na kunywa mezani pangu katika karamu ya ufalme wangu, na kukaa katika viti vya enzi, mkihukumu makabila kumi na mawili ya Israeli.” Yesu akasema, “Simoni, Simoni, sikiliza, Shetani ameomba kuwapepeta ninyi wote kama ngano. Lakini nimekuombea wewe Simoni ili imani yako isishindwe, nawe ukiisha kunirudia, uwaimarishe ndugu zako.” Petro akajibu, “Bwana, niko tayari kwenda pamoja nawe gerezani na hata kifoni.” Yesu akamjibu, “Ninakuambia Petro, kabla jogoo hajawika usiku wa leo, utakana mara tatu kwamba hunijui mimi.” Kisha Yesu akawauliza, “Nilipowatuma bila mfuko, wala mkoba, wala viatu, mlipungukiwa na kitu chochote?” Wakajibu, “La, hatukupungukiwa na kitu chochote.” Akawaambia, “Lakini sasa, aliye na mfuko na auchukue, na aliye na mkoba vivyo hivyo. Naye asiye na upanga, auze joho lake anunue mmoja. Kwa sababu, nawaambia, andiko hili lazima litimizwe juu yangu, kwamba, ‘Alihesabiwa pamoja na wakosaji’; kwa kweli yaliyoandikwa kunihusu mimi hayana budi kutimizwa.” Wanafunzi wake wakamwambia, “Bwana, tazama hapa kuna panga mbili.” Akawajibu, “Inatosha.”