Luka 2:1-17
Luka 2:1-17 BHN
Siku zile, tangazo rasmi lilitolewa na Kaisari Augusto kuwataka watu wote nchini kote wahesabiwe. Sensa hiyo ilikuwa mara ya kwanza, wakati Kurenio alipokuwa mkuu wa mkoa wa Siria. Basi, wote waliohusika walikwenda kuhesabiwa kila mtu katika mji wake. Yosefu pia alifanya safari kutoka mjini Nazareti mkoani Galilaya, na kwa vile alikuwa wa jamaa na ukoo wa Daudi, alikwenda mjini Bethlehemu mkoani Yudea, alikozaliwa mfalme Daudi. Alikwenda kuhesabiwa pamoja na mchumba wake Maria ambaye alikuwa mjamzito. Walipokuwa huko, siku yake ya kujifungua ikawadia, akajifungua mtoto wake wa kwanza wa kiume, akamvika nguo za kitoto, akamlaza horini kwa sababu hawakupata nafasi katika nyumba ya wageni. Katika sehemu hizo, walikuwako wachungaji wakikesha usiku mbugani kulinda mifugo yao. Malaika wa Bwana akawatokea ghafla, na utukufu wa Bwana ukawaangazia pande zote. Wakaogopa sana. Malaika akawaambia, “Msiogope! Nimewaleteeni habari njema ya furaha kubwa itakayowapata watu wote. Kwa maana, leo hii katika mji wa Daudi, amezaliwa Mwokozi kwa ajili yenu, ndiye Kristo Bwana. Na hiki kitakuwa kitambulisho kwenu: Mtamkuta mtoto mchanga amevikwa nguo za kitoto, amelazwa horini.” Mara kundi kubwa la jeshi la mbinguni likajiunga na huyo malaika, wakamsifu Mungu wakisema: “Utukufu kwa Mungu juu mbinguni, na amani duniani kwa watu anaowafadhili!” Baada ya hao malaika kuondoka na kurudi mbinguni, wachungaji wakaambiana: “Twendeni moja kwa moja mpaka Bethlehemu tukalione tukio hili Bwana alilotujulisha.” Basi, wakaenda mbio, wakamkuta Maria na Yosefu na yule mtoto mchanga amelazwa horini. Hao wachungaji walipomwona mtoto huyo wakawajulisha wote habari waliyokuwa wamesikia juu yake.