Luka 18:19-34
Luka 18:19-34 BHN
Yesu akamwambia, “Mbona waniita mwema? Hakuna aliye mwema ila Mungu peke yake. Unazijua amri: ‘Usizini; Usiue; Usiibe; Usitoe ushahidi wa uongo; Waheshimu baba yako na mama yako.’” Yeye akasema, “Hayo yote nimeyazingatia tangu ujana wangu.” Yesu aliposikia hayo, akamwambia, “Unatakiwa bado kufanya kitu kimoja: Uza kila kitu ulicho nacho, wagawie maskini hiyo fedha, nawe utakuwa na hazina yako mbinguni; halafu njoo unifuate.” Lakini huyo mtu aliposikia hayo, alihuzunika sana kwa sababu alikuwa tajiri sana. Yesu alipoona akihuzunika hivyo, akasema, “Jinsi gani ilivyo vigumu kwa matajiri kuingia katika ufalme wa Mungu! Naam, ni rahisi zaidi kwa ngamia kupita katika tundu la sindano, kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu.” Wale watu waliposikia hayo, wakasema, “Nani basi, atakayeokolewa?” Yesu akajibu, “Yasiyowezekana kwa binadamu, yanawezekana kwa Mungu.” Naye Petro akamwuliza, “Na sisi, je? Tumeacha vitu vyote tukakufuata!” Yesu akawaambia, “Kweli nawaambieni, mtu yeyote aliyeacha nyumba au mke au ndugu au wazazi au watoto kwa ajili ya ufalme wa Mungu, atapokea mengi zaidi wakati huu wa sasa, na uhai wa milele wakati ujao.” Yesu aliwachukua kando wale kumi na wawili, akawaambia, “Sikilizeni! Tunakwenda Yerusalemu na huko kila kitu kilichoandikwa na manabii kuhusu Mwana wa Mtu kitakamilishwa. Kwa maana atakabidhiwa kwa watu wa mataifa nao watamtendea vibaya na kumtemea mate. Watampiga mijeledi na kumuua; lakini siku ya tatu atafufuka.” Lakini wao hawakuelewa jambo hilo hata kidogo; walikuwa wamefichwa maana ya maneno hayo, na hawakutambua yaliyosemwa.