Luka 18:19-34
Luka 18:19-34 SRUV
Yesu akamwambia, Mbona unaniita mwema? Hakuna aliye mwema ila mmoja, naye ndiye Mungu. Wazijua amri; Usizini, Usiue, Usiibe, Usishuhudie uongo, Waheshimu baba yako na mama yako. Akasema, Hayo yote nimeyashika tangu utoto wangu. Yesu aliposikia hayo alimwambia, Umepungukiwa na neno moja bado; viuze ulivyo navyo vyote, ukawagawie maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha, njoo unifuate. Lakini aliposikia hayo alihuzunika sana, maana alikuwa na mali nyingi. Yesu alipoona vile alisema, Kwa shida gani wenye mali watauingia ufalme wa Mungu! Kwa maana ni rahisi ngamia kupita katika tundu la sindano kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu. Nao waliosikia walisema, Ni nani basi awezaye kuokoka? Akasema, Yasiyowezekana kwa wanadamu yawezekana kwa Mungu. Petro akasema, Tazama, sisi tumeviacha vitu vyetu vyote na kukufuata. Akawaambia, Hakika nawaambia, hakuna mtu aliyeacha nyumba, au mke, au ndugu, au wazazi, au wana, kwa ajili ya ufalme wa Mungu, asiyepokea zaidi mara nyingi katika wakati huu, na katika ulimwengu ujao uzima wa milele. Akawachukua wale Kumi na Wawili, akawaambia, Tazameni, tunapanda kwenda Yerusalemu, na mambo yote, Mwana wa Adamu aliyoandikiwa na manabii yatatimizwa. Kwa kuwa atatiwa mikononi mwa Mataifa, atafanyiwa dhihaka; atatendwa jeuri, na kutemewa mate; nao watampiga mijeledi, kisha watamwua; na siku ya tatu atafufuka. Lakini hawakuelewa maneno hayo hata kidogo, na jambo hilo lilikuwa limefichwa kwao, wala hawakufahamu yaliyonenwa.