Luka 1:57-80
Luka 1:57-80 BHN
Wakati wa kujifungua kwake Elisabeti ulifika, akajifungua mtoto wa kiume. Jirani na watu wa jamaa yake walipopata habari kwamba Bwana amemwonea huruma kubwa, walifurahi pamoja naye. Halafu siku ya nane walifika kumtahiri mtoto, wakataka kumpa jina la baba yake, Zakaria. Lakini mama yake akasema, “Sivyo, bali ataitwa Yohane.” Wakamwambia, “Mbona hakuna yeyote katika ukoo wake mwenye jina hilo?” Basi, wakamwashiria baba yake wapate kujua alitaka mtoto wake apewe jina gani. Naye akaomba kibao cha kuandikia, akaandika hivi: “Yohane ndilo jina lake.” Wote wakastaajabu. Papo hapo, midomo na ulimi wake Zakaria vikafunguliwa, akawa anaongea akimsifu Mungu. Hofu ikawaingia jirani wote, na habari hizo zikaenea kila mahali katika milima ya Yudea. Wote waliosikia mambo hayo, waliyatafakari mioyoni mwao wakisema: “Mtoto huyu atakuwa mtu wa namna gani?” Maana, hakika nguvu ya Bwana ilikuwa pamoja naye. Zakaria, baba yake mtoto, akajazwa Roho Mtakatifu, akatamka unabii huu: “Atukuzwe Bwana Mungu wa Israeli, kwani amewajia na kuwakomboa watu wake. Ametupatia Mwokozi shujaa, mzawa wa Daudi mtumishi wake. Aliahidi hapo kale kwa njia ya manabii wake watakatifu, kwamba atatuokoa mikononi mwa maadui zetu na kutoka mikononi mwa wote wanaotuchukia. Alisema atawahurumia wazee wetu, na kukumbuka agano lake takatifu. Alimwapia Abrahamu babu yetu, kwamba atatujalia sisi tukombolewe mikononi mwa maadui zetu, tupate kumtumikia bila hofu, tuwe wanyofu na waadilifu mbele yake, siku zote za maisha yetu. Nawe mwanangu, utaitwa, nabii wa Mungu Mkuu, utamtangulia Bwana kumtayarishia njia yake; kuwatangazia watu kwamba wataokolewa kwa kuondolewa dhambi zao. Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma. Atatuchomozea mwanga kutoka juu, na kuwaangazia wote wanaokaa katika giza kuu la kifo, aongoze hatua zetu katika njia ya amani.” Mtoto akakua, akapata nguvu rohoni. Alikaa jangwani mpaka alipojionesha rasmi kwa watu wa Israeli.