Luka 1:57-80
Luka 1:57-80 NENO
Ulipowadia wakati wa Elizabeti kujifungua, alizaa mtoto wa kiume. Majirani zake na jamii zake wakasikia jinsi Mwenyezi Mungu alivyomfanyia rehema kuu, nao wakafurahi pamoja naye. Siku ya nane wakaja kumtahiri mtoto, wakataka yule mtoto aitwe Zakaria, ambalo ndilo jina la baba yake. Lakini mama yake akakataa na kusema, “Hapana! Jina lake ataitwa Yahya.” Wakamwambia, “Hakuna mtu yeyote katika jamaa yako mwenye jina kama hilo.” Basi wakamfanyia Zakaria baba yake ishara ili kujua kwamba yeye angependa kumpa mtoto jina gani. Akaomba wampe kibao cha kuandikia na kwa mshangao wa kila mtu akaandika: “Jina lake ni Yahya.” Papo hapo kinywa chake kikafunguliwa na ulimi wake pia, akaanza kuongea, huku akimsifu Mungu. Majirani wote wakajawa na hofu ya Mungu, na katika nchi yote ya vilima ya Yudea watu walikuwa wakinena kuhusu mambo haya yote. Kila aliyesikia habari hizi alishangaa akauliza, “Je, mtoto huyu atakuwa mtu wa namna gani?” Maana mkono wa Mwenyezi Mungu ulikuwa pamoja naye. Zakaria, baba yake, akajazwa na Roho Mtakatifu wa Mungu, naye akatoa unabii, akisema: “Ahimidiwe Bwana, Mungu wa Israeli, kwa kuwa amewajilia watu wake na kuwakomboa. Naye ametusimamishia pembe ya wokovu katika nyumba ya Daudi mtumishi wake, (kama alivyonena kwa vinywa vya manabii wake watakatifu tangu zamani), kwamba atatuokoa kutoka kwa adui zetu, na kutoka mikononi mwao wote watuchukiao: ili kuonesha rehema kwa baba zetu na kukumbuka agano lake takatifu, kiapo alichomwapia baba yetu Ibrahimu: kutuokoa kutoka mikononi mwa adui zetu, tupate kumtumikia yeye pasipo hofu katika utakatifu na haki mbele zake, siku zetu zote. “Nawe mtoto wangu, utaitwa nabii wa Aliye Juu Sana; kwa kuwa utamtangulia Mwenyezi Mungu na kuandaa njia kwa ajili yake, kuwajulisha watu wake wokovu utakaopatikana kwa kusamehewa dhambi zao, kwa ajili ya wingi wa rehema za Mungu wetu, nuru inayotoka juu itatuzukia ili kuwaangazia wale wanaoishi gizani na katika uvuli wa mauti, kuiongoza miguu yetu katika njia ya amani.” Yule mtoto akakua na kuongezeka nguvu katika roho; akaishi nyikani hadi siku ile alipojionesha hadharani kwa Waisraeli.