Walawi 23:1-8
Walawi 23:1-8 BHN
Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Waambie Waisraeli hivi: Katika sikukuu zangu mimi Mwenyezi-Mungu ambazo zimepangwa mtakuwa na mkutano mtakatifu. Sikukuu ambazo nimepanga ni hizi: Kutakuwa na siku sita za kufanya kazi. Lakini siku ya saba ni Sabato; siku hiyo ni ya mapumziko rasmi, hamtafanya kazi na mtakuwa na mkutano mtakatifu. Siku hiyo ya saba hamtafanya kazi; hiyo ni Sabato ambayo ni wakfu kwangu mimi Mwenyezi-Mungu katika makao yenu yote. “Sikukuu zangu nyingine mimi Mwenyezi-Mungu ambazo mtakuwa na mkutano mtakatifu zitafanyika katika nyakati zifuatazo zilizopangwa. “Jioni ya siku ya kumi na nne ya mwezi wa kwanza mtaadhimisha kwa heshima yangu mimi Mwenyezi-Mungu sikukuu ya Pasaka. Siku ya kumi na tano ya mwezi huohuo, sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu itaanza. Kwa muda wa siku saba, mtakula mikate isiyotiwa chachu. Katika siku ya kwanza mtakuwa na mkutano mtakatifu. Siku hiyo msifanye kazi. Kwa muda wa siku hizo zote saba mtanitolea mimi Mwenyezi-Mungu sadaka za kuteketezwa kwa moto. Katika siku ya saba mtafanya mkutano mtakatifu. Msifanye kazi.”