Walawi 23:1-8
Walawi 23:1-8 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Waambie Waisraeli hivi: Katika sikukuu zangu mimi Mwenyezi-Mungu ambazo zimepangwa mtakuwa na mkutano mtakatifu. Sikukuu ambazo nimepanga ni hizi: Kutakuwa na siku sita za kufanya kazi. Lakini siku ya saba ni Sabato; siku hiyo ni ya mapumziko rasmi, hamtafanya kazi na mtakuwa na mkutano mtakatifu. Siku hiyo ya saba hamtafanya kazi; hiyo ni Sabato ambayo ni wakfu kwangu mimi Mwenyezi-Mungu katika makao yenu yote. “Sikukuu zangu nyingine mimi Mwenyezi-Mungu ambazo mtakuwa na mkutano mtakatifu zitafanyika katika nyakati zifuatazo zilizopangwa. “Jioni ya siku ya kumi na nne ya mwezi wa kwanza mtaadhimisha kwa heshima yangu mimi Mwenyezi-Mungu sikukuu ya Pasaka. Siku ya kumi na tano ya mwezi huohuo, sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu itaanza. Kwa muda wa siku saba, mtakula mikate isiyotiwa chachu. Katika siku ya kwanza mtakuwa na mkutano mtakatifu. Siku hiyo msifanye kazi. Kwa muda wa siku hizo zote saba mtanitolea mimi Mwenyezi-Mungu sadaka za kuteketezwa kwa moto. Katika siku ya saba mtafanya mkutano mtakatifu. Msifanye kazi.”
Walawi 23:1-8 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia, Nena na wana wa Israeli, na kuwaambia, Sikukuu za BWANA, ambazo mtazitangaza kuwa ni makusanyiko matakatifu; hizi ni sikukuu zangu. Mtafanya kazi siku sita; lakini siku ya saba ni Sabato ya kustarehe kabisa, kusanyiko takatifu; msifanye kazi ya namna yoyote; ni Sabato kwa BWANA katika makao yenu yote. Sikukuu za BWANA ni hizi, ni makusanyiko matakatifu, ambayo mtayatangaza kwa nyakati zake. Mwezi wa kwanza, siku ya kumi na nne ya mwezi wakati wa jioni, ni Pasaka ya BWANA. Na siku ya kumi na tano ya mwezi ule ule ni sikukuu kwa BWANA ya mkate usiotiwa chachu; mtaila mikate isiyochachwa muda wa siku saba. Siku ya kwanza mtakuwa na kusanyiko takatifu msifanye kazi yoyote ya utumishi. Lakini mtasongeza sadaka kwa BWANA kwa njia ya moto siku saba; siku ya saba ni kusanyiko takatifu; msifanye kazi yoyote ya utumishi.
Walawi 23:1-8 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia, Nena na wana wa Israeli, na kuwaambia, Sikukuu za BWANA, ambazo mtazipigia mbiu kuwa ni makusanyiko matakatifu; hizi ni sikukuu zangu. Mtafanya kazi siku sita; lakini siku ya saba ni Sabato ya kustarehe kabisa, kusanyiko takatifu; msifanye kazi ya namna yo yote; ni Sabato kwa BWANA katika makao yenu yote. Sikukuu za BWANA ni hizi, ni makusanyiko matakatifu, ambayo mtayapigia mbiu kwa nyakati zake. Mwezi wa kwanza, siku ya kumi na nne ya mwezi wakati wa jioni, ni pasaka ya BWANA. Na siku ya kumi na tano ya mwezi ule ule ni sikukuu kwa BWANA ya mkate usiotiwa chachu; mtaila mikate isiyochachwa muda wa siku saba. Siku ya kwanza mtakuwa na kusanyiko takatifu msifanye kazi yo yote ya utumishi. Lakini mtasongeza sadaka kwa BWANA kwa njia ya moto siku saba; siku ya saba ni kusanyiko takatifu; msifanye kazi yo yote ya utumishi.
Walawi 23:1-8 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Sema na Waisraeli na uwaambie: ‘Hizi ndizo sikukuu zangu zilizoamriwa, sikukuu zilizoamriwa za Mwenyezi Mungu, ambazo mtazitangaza kuwa makusanyiko matakatifu. “ ‘Kuna siku sita mnazoweza kufanya kazi, lakini siku ya saba ni Sabato ya kupumzika, siku ya kusanyiko takatifu. Hamtafanya kazi yoyote. Popote mnapoishi, ni Sabato kwa Mwenyezi Mungu. “ ‘Hizi ni sikukuu za Mwenyezi Mungu zilizoamriwa, makusanyiko matakatifu mtakayoyatangaza kwa nyakati zilizoamriwa: Pasaka ya Mwenyezi Mungu huanza jioni ya siku ya kumi na nne ya mwezi wa kwanza. Siku ya kumi na tano ya mwezi huo wa kwanza, Sikukuu ya Mwenyezi Mungu ya Mikate Isiyotiwa Chachu huanza; kwa siku saba, mtakula mikate isiyotiwa chachu. Katika siku ya kwanza, mtakuwa na kusanyiko takatifu, na msifanye kazi zenu za kawaida. Kwa siku saba mtamletea Mwenyezi Mungu sadaka ya kuteketezwa kwa moto. Kwenye siku hiyo ya saba mtafanya kusanyiko takatifu, na msifanye kazi zenu za kawaida.’ ”