Walawi 10:1-7
Walawi 10:1-7 BHN
Nao Nadabu na Abihu, wanawe Aroni, walichukua kila mmoja chetezo chake, wakaweka moto na ubani, wakamtolea Mwenyezi-Mungu moto najisi, ambao haukulingana na agizo lake Mwenyezi-Mungu. Basi, moto ukatokea mbele ya Mwenyezi-Mungu, ukawateketeza hao vijana, wakafa mbele yake. Hapo, Mose akamwambia Aroni, “Kwa tukio hili Mwenyezi-Mungu amekuonesha maana ya kile alichosema: ‘Nitajionesha kuwa mtakatifu miongoni mwa wale walio karibu nami; nitatukuzwa mbele ya watu wote!’” Aroni akanyamaza kimya. Basi, Mose akawaita Mishaeli na Elsafani, wanawe Uzieli, baba mdogo wa Aroni, akawaambia waje kuondoa maiti za ndugu zao maskani na kuzipeleka nje ya kambi. Wakachukua maiti za ndugu zao na kuzipeleka nje ya kambi wakiwa wamevaa mavazi yao, kama Mose alivyoamuru. Kisha Mose akamwambia Aroni na wanawe, Eleazari na Ithamari, “Msivuruge nywele zenu na wala msirarue mavazi yenu kuomboleza, la sivyo mtakufa na kuiletea jumuiya yote ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu. Lakini ndugu zenu yaani jumuiya yote ya Israeli, wanaweza kuomboleza kwa sababu ya moto huo aliouleta Mwenyezi-Mungu. Msitoke nje ya mlango wa hema la mkutano, la sivyo mtakufa; kwani mafuta ya kupaka ya Mwenyezi-Mungu yangali juu yenu.” Aroni na wanawe wakafanya kama Mose alivyosema.