Mambo ya Walawi 10:1-7
Mambo ya Walawi 10:1-7 SRUV
Na Nadabu na Abihu, wana wa Haruni, wakatwaa kila mtu chetezo chake, wakatia moto ndani yake, wakatia na uvumba, nao wakatoa moto najisi mbele ya BWANA, ambao yeye hakuwaagiza. Kisha moto ukatoka hapo mbele za BWANA, na ukawateketeza, nao wakafa mbele za BWANA. Ndipo Musa akamwambia Haruni, Jambo hili ni hilo BWANA alilolinena, akisema, Nitatakaswa mimi katika hao wanikaribiao, nami nitatukuzwa mbele ya watu hao wote. Haruni akanyamaza kimya. Musa akawaita Mishaeli na Elisafani, wana wa Uzieli mjombaye Haruni, na kuwaambia, Njoni karibu, mwachukue hawa ndugu zenu, mkawaondoe hapa mbele ya maskani, mwende nao nje ya kambi. Basi wakaja karibu, na kuwachukua, wakiwa wamevaa nguo zao, wakawachukua nje ya kambi; kama Musa alivyosema. Kisha Musa akamwambia Haruni na wanawe Eleazari na Ithamari, Msiache wazi nywele za vichwani mwenu, wala msiyararue mavazi yenu; ili kwamba msife, tena asiukasirikie mkutano wote; lakini ndugu zenu, nyumba yote ya Israeli, na waomboleze kwa ajili ya waliochomwa na moto wa BWANA. Wala hamtatoka nje mlangoni mwa hema ya kukutania, msije mkafa; kwa sababu mafuta ya kutiwa ya BWANA yako juu yenu. Nao wakafanya kama hilo neno la Musa.