Maombolezo 3:45-66
Maombolezo 3:45-66 BHN
Umetufanya kuwa takataka na uchafu miongoni mwa watu wa mataifa. “Maadui zetu wote wanatuzomea. Kitisho na hofu vimetuandama, tumepatwa na maafa na maangamizi. Macho yangu yabubujika mito ya machozi kwa sababu ya kuangamizwa kwa watu wangu. “Machozi yatanitoka bila kikomo, mpaka Mwenyezi-Mungu kutoka huko mbinguni aangalie chini na kuona. Nalia na kujaa majonzi, kuona yaliyowapata kina mama wa mji wangu. “Nimewindwa kama ndege na hao wanichukiao bila sababu. Walinitupa shimoni nikiwa hai na juu yangu wakarundika mawe. Maji yalianza kunifunika kichwa, nami nikafikiri, ‘Huu ni mwisho wangu.’ “Kutoka chini shimoni nilikulilia ee Mwenyezi-Mungu. Wewe umenisikia nikikulilia: ‘Usiache kusikia kilio changu cha msaada bali unipatie nafuu.’ Nilipokuita ulinijia karibu ukaniambia, ‘Usiogope!’ “Umenitetea katika kisa changu ee Mwenyezi-Mungu, umeyakomboa maisha yangu. Umeuona uovu niliotendewa ee Mwenyezi-Mungu, uniamulie kwa wema kisa changu. Umeuona uovu wa maadui zangu, na mipango yao yote ya hila dhidi yangu. “Umesikia matukano yao ee Mwenyezi-Mungu, na mipango yao yote ya hila dhidi yangu. Maneno na mawazo ya maadui zangu siku nzima ni juu ya kuniangamiza mimi. Wakati wote, wamekaa au wanakwenda, mimi ndiye wanayemzomea. Uwalipize, ee Mwenyezi-Mungu kadiri ya hayo matendo yao, kadiri ya mambo waliyotenda wenyewe. Uipumbaze mioyo yao, na laana yako iwashukie. Uwafuatie kwa hasira, uwaangamize, uwafanye watoweke ulimwenguni.”