Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Maombolezo 1:12-22

Maombolezo 1:12-22 BHN

“Enyi wapita njia, hivi hamjali kitu? Tazameni! Hakuna aliyepatwa na uchungu kama mimi, uchungu alioniletea Mwenyezi-Mungu, siku ya hasira yake kali. “Aliteremsha moto kutoka juu, ukanichoma hata mifupani mwangu. Alinitegea wavu akaninasa, kisha akanirudisha nyuma, akaniacha nimeduwaa na kuzirai mchana kutwa. “Aliyahesabu makosa yangu yote akayakusanya mahali pamoja; aliyafunga shingoni mwangu kama nira, nikafyonzwa nguvu zangu kwa uzito wake. Mwenyezi-Mungu aliniweka mikononi mwao watu ambao siwezi kuwapinga. “Mwenyezi-Mungu aliwakataa askari walionilinda, alitangaza wakati maalumu wa kuniadhibu kuwaponda vijana wangu wa kiume. Aliwaponda kama katika shinikizo watu wangu wa Yuda. “Kwa sababu ya hayo ninalia, machozi yanitiririka, sina mtu yeyote wa kunifariji; hakuna yeyote wa kunitia moyo. Watoto wangu wameachwa wakiwa, maana adui yangu amenishinda. “Nainyosha mikono yangu lakini hakuna wa kunifariji. Mwenyezi-Mungu ametoa amri dhidi yangu mimi Yakobo, jirani zangu wawe maadui zangu. Naam, mimi Yerusalemu nimekuwa kinyaa kwao. “Lakini Mwenyezi-Mungu amefanya sawa kwa maana nimeliasi neno lake. Nisikilizeni enyi watu wote, yatazameni mateso yangu. Wasichana wangu na wavulana wangu, wamechukuliwa mateka. “Niliwaita wapenzi wangu, lakini wao wakanihadaa. Makuhani na wazee wangu wamefia mjini wakijitafutia chakula, ili wajirudishie nguvu zao. “Ona, ee Mwenyezi-Mungu nilivyo taabuni. Roho yangu imechafuka, moyo wangu unasononeka kwani nimekuasi vibaya. Huko nje kumejaa mauaji, ndani nako ni kama kifo tu. “Sikiliza ninavyopiga kite; hakuna wa kunifariji. Maadui zangu wote wamesikia juu ya taabu yangu: Wanafurahi kwamba umeniletea maafa. Uifanye ile siku uliyoahidi ifike, uwafanye nao wateseke kama mimi. “Uwapatilize kwa ajili ya uovu wao wote. Uwatende kama ulivyonitenda mimi kwa sababu ya makosa yangu yote. Nasononeka sana kwa maumivu na moyo wangu unazimia.”