Omb 1:12-22
Omb 1:12-22 SUV
Je! Si kitu kwenu, enyi nyote mpitao njia, Angalieni, mtazame Kama kuna majonzi yo yote mfano wa majonzi yangu, Niliyotendwa mimi, Ambayo BWANA amenihuzunisha kwa hayo Siku ya hasira yake iwakayo. Toka juu amepeleka moto mifupani mwangu, Nao umeishinda; Ametandika wavu aninase miguu, Amenirudisha nyuma; Amenifanya kuwa mtu wa pekee, Na mgonjwa mchana kutwa. Kongwa la makosa yangu limefungwa na mkono wake; Hayo yameshikamana; Yamepanda juu shingoni mwangu; Amezikomesha nguvu zangu; Bwana amenitia mikononi mwao, Ambao siwezi kupingamana nao. Bwana amewafanya mashujaa wangu wote Kuwa si kitu kati yangu; Ameita mkutano mkuu kinyume changu Ili kuwaponda vijana wangu; Bwana amemkanyaga kama shinikizoni Huyo bikira binti Yuda. Mimi ninayalilia mambo hayo; Jicho langu, jicho langu linachuruzika maji; Kwa kuwa mfariji yu mbali nami, Ambaye ilimpasa kunihuisha nafsi; Watoto wangu wameachwa peke yao, Kwa sababu huyo adui ameshinda. Sayuni huinyosha mikono yake; Hakuna hata mmoja wa kumfariji; BWANA ametoa amri juu ya Yakobo, Kwamba wamzungukao wawe watesi wake; Yerusalemu amekuwa kati yao Kama kitu kichafu. BWANA ndiye mwenye haki; Maana nimeiasi amri yake; Sikieni, nawasihi, enyi watu wote, Mkayatazame majonzi yangu; Wasichana wangu na wavulana wangu Wamechukuliwa mateka. Naliwaita hao walionipenda Lakini walinidanganya; Makuhani wangu na wazee wangu Walifariki mjini; Hapo walipokuwa wakitafuta chakula ili kuzihuisha nafsi zao. Angalia, Ee BWANA; maana mimi ni katika dhiki; Mtima wangu umetaabika; Moyo wangu umegeuka ndani yangu; Maana nimeasi vibaya sana; Huko nje upanga hufisha watu; Nyumbani mna kama mauti. Wamesikia kwamba napiga kite; Hakuna hata mmoja wa kunifariji; Adui zangu wote wamesikia habari ya mashaka yaliyonipata; Hufurahi kwa kuwa umeyafanya hayo; Utaileta siku ile uliyoitangaza, Nao watakuwa kama mimi. Huo uovu wao wote Na uje mbele zako wewe; Ukawatende wao kama ulivyonitenda mimi Kwa dhambi zangu zote; Kwa maana mauguzi yangu ni mengi sana, Na moyo wangu umezimia.