Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yoshua 6:20-27

Yoshua 6:20-27 BHN

Basi, watu wakapiga kelele huku mabaragumu yanapigwa. Watu waliposikia sauti ya mabaragumu walipiga kelele kubwa, na kuta za mji zikaanguka chini kabisa. Mara watu wakauvamia mji, kila mmoja kutoka mahali aliposimama, wakauteka. Kisha wakaangamiza kila kitu mjini humo na kuwaua kwa upanga: Wanaume na wanawake, vijana na wazee, ng'ombe, kondoo na punda. Yoshua akawaambia wale wapelelezi wawili walioipeleleza nchi hiyo, “Nendeni katika nyumba ya yule kahaba; mkamlete yule mwanamke na wale wote ambao ni ndugu zake kama mlivyomwapia.” Basi, wale vijana wapelelezi wakaenda; wakamleta Rahabu, baba yake na mama yake, ndugu zake na watu wote wa jamaa yake, wakawaweka nje ya kambi ya Israeli. Kisha, wakauchoma moto mji wa Yeriko na kila kitu kilichokuwako isipokuwa fedha, dhahabu, vyombo vya shaba na vya chuma; hivyo viliwekwa katika hazina ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Lakini yule kahaba Rahabu pamoja na watu wote wa nyumba ya baba yake, Yoshua aliyaokoa maisha yao. Rahabu akaishi miongoni mwa Waisraeli hadi leo, kwa kuwa aliwaficha wajumbe ambao Yoshua aliwatuma kwenda kuupeleleza mji wa Yeriko. Wakati huo Yoshua alitamka apizo rasmi mbele ya watu akisema, “Atakayeujenga tena mji wa Yeriko, na alaaniwe na Mungu, Yeyote atakayeweka msingi wa mji huo, mzaliwa wake wa kwanza na afe. Yeyote atakayejenga lango la mji huo, mwanawe kitinda mimba na afe.” Basi, Mwenyezi-Mungu alikuwa pamoja na Yoshua na sifa zake zikaenea nchini kote.

Soma Yoshua 6