Yos 6:20-27
Yos 6:20-27 SUV
Basi watu wakapiga kelele, na makuhani wakazipiga tarumbeta; hata ikawa, hapo watu waliposikia sauti ya tarumbeta hao watu wakapiga kelele kwa sauti kuu sana, na ule ukuta wa mji ukaanguka nchi kabisa, hata watu wakapanda juu, wakaingia katika mji, kila mtu akiendelea kukabili mbele; wakautwaa huo mji. Basi wakaangamiza kabisa vitu vyote vilivyokuwa ndani ya mji, wanaume na wanawake, watoto na wazee, na ng’ombe, na kondoo, na punda, kwa makali ya upanga. Naye Yoshua akawaambia wale wanaume wawili walioipeleleza nchi, Ingieni katika nyumba ya yule kahaba, mkamtoe huyo mwanamke mwenyewe na vitu vyote alivyo navyo, kama mlivyomwapia. Basi wale vijana wapelelezi wakaingia, wakamtoa Rahabu, na baba yake, na mama yake, na ndugu zake, na vitu vyote walivyokuwa navyo, wakawatoa na jamaa zake wote pia; wakawaweka nje ya matuo ya Israeli. Kisha wakauteketeza mji kwa moto, na vitu vyote vilivyokuwa ndani yake; bali fedha, na dhahabu, na vyombo vya shaba, na vya chuma, wakavitia katika hazina ya nyumba ya BWANA. Lakini Yoshua akamhifadhi Rahabu, yule kahaba, na watu wa nyumba ya baba yake, na vitu vyote alivyokuwa navyo; naye akakaa kati ya Israeli hata leo; kwa sababu aliwaficha wale wajumbe aliowatuma Yoshua ili kuupeleleza mji wa Yeriko. Naye Yoshua akawaapisha kiapo wakati ule, akasema, Na alaaniwe mbele za BWANA mtu yule atakayeinuka na kuujenga tena mji huu wa Yeriko; ataweka msingi wake kwa kufiliwa na mzaliwa wa kwanza wake, tena atayasimamisha malango yake kwa kufiliwa na mtoto wake mwanamume aliye mdogo. Basi BWANA alikuwa pamoja na Yoshua; sifa zake zikaenea katika nchi ile yote.