Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yobu 39:13-30

Yobu 39:13-30 BHN

“Mbuni hupigapiga mabawa yake kwa madaha, lakini hawezi kuruka kama korongo. Mbuni huyaacha mayai yake juu ya ardhi ili yapate joto mchangani; lakini hajui kama yanaweza kukanyagwa, au kuvunjwa na mnyama wa porini. Mbuni huwatendea wanawe ukatili kama si wake, hata kazi yake ikiharibika yeye hana wasiwasi; kwa sababu nilimfanya asahau hekima yake, wala sikumpa sehemu yoyote ya akili. Lakini akianza kukimbia, humcheka hata farasi na mpandafarasi. “Je, Yobu, ndiwe uliyewapa farasi nguvu, ukawavika shingoni manyoya marefu? Je, ni wewe unayemfanya farasi aruke kama nzige? Mlio wake wa maringo ni wa ajabu! Huparapara ardhi mabondeni kwa pupa; hukimbilia kwenye mapigano kwa nguvu zake zote. Farasi huicheka hofu, na hatishiki; wala upanga hauwezi kumrudisha nyuma. Silaha wachukuazo wapandafarasi, hugongana kwa sauti na kungaa juani. Farasi husonga mbele, akitetemeka kwa hasira; tarumbeta iliapo, yeye hasimami. Kila ipigwapo tarumbeta, yeye hutoa sauti; huisikia harufu ya vita toka mbali, huusikia mshindo wa makamanda wakitoa amri kwa makelele. “Je, mwewe amejifunza kwako jinsi ya kuruka, na kunyosha mabawa yake kuelekea kusini? Je, tai hupaa juu kwa amri yako, na kuweka kiota chake juu milimani? Tai hufanya makazi yake juu ya miamba mirefu, na ncha kali za majabali ndizo ngome zake. Kutoka huko huotea mawindo, macho yake huyaona kutoka mbali. Makinda yake hufyonza damu; pale ulipo mzoga ndipo alipo tai.”

Soma Yobu 39