Yobu 39:13-30
Yobu 39:13-30 Biblia Habari Njema (BHN)
“Mbuni hupigapiga mabawa yake kwa madaha, lakini hawezi kuruka kama korongo. Mbuni huyaacha mayai yake juu ya ardhi ili yapate joto mchangani; lakini hajui kama yanaweza kukanyagwa, au kuvunjwa na mnyama wa porini. Mbuni huwatendea wanawe ukatili kama si wake, hata kazi yake ikiharibika yeye hana wasiwasi; kwa sababu nilimfanya asahau hekima yake, wala sikumpa sehemu yoyote ya akili. Lakini akianza kukimbia, humcheka hata farasi na mpandafarasi. “Je, Yobu, ndiwe uliyewapa farasi nguvu, ukawavika shingoni manyoya marefu? Je, ni wewe unayemfanya farasi aruke kama nzige? Mlio wake wa maringo ni wa ajabu! Huparapara ardhi mabondeni kwa pupa; hukimbilia kwenye mapigano kwa nguvu zake zote. Farasi huicheka hofu, na hatishiki; wala upanga hauwezi kumrudisha nyuma. Silaha wachukuazo wapandafarasi, hugongana kwa sauti na kungaa juani. Farasi husonga mbele, akitetemeka kwa hasira; tarumbeta iliapo, yeye hasimami. Kila ipigwapo tarumbeta, yeye hutoa sauti; huisikia harufu ya vita toka mbali, huusikia mshindo wa makamanda wakitoa amri kwa makelele. “Je, mwewe amejifunza kwako jinsi ya kuruka, na kunyosha mabawa yake kuelekea kusini? Je, tai hupaa juu kwa amri yako, na kuweka kiota chake juu milimani? Tai hufanya makazi yake juu ya miamba mirefu, na ncha kali za majabali ndizo ngome zake. Kutoka huko huotea mawindo, macho yake huyaona kutoka mbali. Makinda yake hufyonza damu; pale ulipo mzoga ndipo alipo tai.”
Yobu 39:13-30 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Bawa la mbuni hufurahi; Lakini mabawa yake na manyoya yake, je! Yana huruma? Kwa maana yeye huyaacha mayai yake juu ya nchi, Na kuyatia moto mchangani, Na kusahau kwamba huenda mguu ukayavunja, Au mnyama-pori kuyakanyaga. Yeye huwatendea ukatili makinda yake, kama kwamba si yake; Ijapokuwa kazi yake yaweza kuwa ya bure, yeye hana hofu; Kwa sababu Mungu amemnyima akili, Wala hakumpa fahamu. Wakati anapojiinua juu aende, Humdharau farasi na mwenye kumpanda. Je! Wewe ulimpa farasi uwezo wake? Au, ni wewe uliyemvika shingo yake manyoya yatetemayo? Ndiwe uliyemfanya aruke kama nzige? Fahari ya mlio wake hutisha. Huparapara bondeni, na kuzifurahia nguvu zake; Hutoka kwenda kukutana na wenye silaha. Yeye hufanyia kicho dhihaka, wala hashangai; Wala hageuki kurudi nyuma mbele ya upanga. Podo humpigia makelele, Mkuki ung'aao na fumo. Huimeza nchi kwa ukali wake na ghadhabu; Wala hasimami kwa sauti ya baragumu. Kila ipigwapo baragumu yeye husema, Aha! Naye husikia harufu ya vita toka mbali, Mshindo wa makamanda, na makelele. Je! Mwewe huruka juu kwa akili zako, Na kuyanyosha mabawa yake kwenda kusini? Je! Tai hupaa juu kwa amri yako, Na kufanya kiota chake mahali pa juu? Hukaa jabalini, ndiko kwenye malazi yake, Juu ya genge la jabali, na ngomeni. Toka huko yeye huchungulia mawindo; Macho yake huyaangalia toka mbali. Makinda yake nayo hufyonza damu; Na pale iliko mizoga ndiko aliko.
Yobu 39:13-30 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Bawa la mbuni hufurahi; Lakini mabawa yake na manyoya yake, je! Yana huruma? Kwani yeye huyaacha mayai yake juu ya nchi, Na kuyatia moto mchangani, Na kusahau kwamba yumkini mguu kuyavunja, Au mnyama wa mwitu kuyakanyaga. yeye huyafanyia ukali makinda yake, kana kwamba si yake; Ijapokuwa taabu yake ni ya bure, hana hofu; Kwa sababu Mungu amemnyima akili, Wala hakumpa fahamu. Wakati anapojiinua juu aende, Humdharau farasi na mwenye kumpanda. Je! Wewe ulimpa farasi uwezo wake? Au, ni wewe uliyemvika shingo yake manyoya yatetemayo? Ndiwe uliyemfanya aruke kama nzige? Fahari ya mlio wake hutisha. Hupara-para bondeni, na kuzifurahia nguvu zake; Hutoka kwenda kukutana na wenye silaha. Yeye hufanyia kicho dhihaka, wala hashangai; Wala hageuki kurudi nyuma mbele ya upanga. Podo humpigia makelele, Mkuki ung’aao na fumo. Huimeza nchi kwa ukali wake na ghadhabu; Wala hasimami kwa sauti ya baragumu. Kila ipigwapo baragumu yeye husema, Aha! Naye husikia harufu ya vita toka mbali, Mshindo wa maakida, na makelele. Je! Mwewe huruka juu kwa akili zako, Na kuyanyosha mabawa yake kwenda kusini? Je! Tai hupaa juu kwa amri yako, Na kufanya kioto chake mahali pa juu? Hukaa jabalini, ndiko kwenye malazi yake, Juu ya genge la jabali, na ngomeni. Toka huko yeye huchungulia mawindo; Macho yake huyaangalia toka mbali. Makinda yake nayo hufyonza damu; Na kwenye maiti ndiko aliko.
Yobu 39:13-30 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
“Mbuni hupigapiga mabawa yake kwa furaha, lakini hayawezi kulinganishwa na mabawa na manyoya ya korongo. Huyataga mayai yake juu ya ardhi, na kuyaacha yapate joto mchangani, bila kujali kuwa mguu waweza kuyaponda, kwamba baadhi ya wanyama wa porini wanaweza kuyakanyaga. Yeye huyafanyia makinda yake ukatili kama vile si yake; hajali kwamba taabu yake inaweza ikawa bure, kwa kuwa Mungu hakumjalia hekima, wala hakumpa fungu la akili njema. Lakini akunjuapo mabawa yake kukimbia, humcheka farasi pamoja na yeye aliyempanda. “Je, wewe humpa farasi nguvu au kuivika shingo yake manyoya marefu? Je, wewe humfanya farasi aruke kama nzige, akistaajabisha kwa tishio la mlio wake wa majivuno? Huparapara bila woga, akizifurahia nguvu zake, husonga mbele kukabiliana na silaha. Huicheka hofu, haogopi chochote, wala haukimbii upanga. Podo hutoa sauti kando yake, pamoja na mkuki unaongʼaa na fumo. Bila woga na kwa ghadhabu huimeza nchi, wala tarumbeta iliapo yeye hawezi kusimama. Asikiapo sauti ya baragumu yeye hulia, ‘Aha!’ Hunusa harufu ya vita toka mbali, sauti ya mtoa amri na ukelele wa vita. “Je, mwewe huruka kwa hekima yako na kuyakunjua mabawa yake kuelekea kusini? Je, tai hupaa juu kwa amri yako na kujenga kiota chake mahali pa juu? Huishi juu ya miamba mirefu na kukaa huko usiku; majabali yenye ncha kali ndiyo ngome yake. Kutoka huko hutafuta chakula chake; macho yake hukiona kutoka mbali. Makinda yake hujilisha damu, na pale palipo na machinjo, ndipo yeye alipo.”