Yobu 29:11-25
Yobu 29:11-25 BHN
Kila aliyesikia habari zangu alinitakia heri na aliponiona, alikubali habari hizo kuwa kweli: Nilimwokoa maskini aliyenililia msaada, kadhalika na yatima asiyekuwa na wa kumsaidia. Waliokuwa karibu kuangamia walinitakia baraka, niliwafanya wajane waone tena furaha moyoni. Uadilifu ulikuwa vazi langu; kutenda haki kulikuwa kama joho na kilemba changu. Kwa vipofu nilikuwa macho ya kuwaonesha njia, kwa viwete nilikuwa miguu yao. Kwa maskini nilikuwa baba yao, nilifanya bidii kutetea haki za watu nisiowajua. Nilizivunja nguvu za watu waovu, nikawafanya wawaachilie mateka wao. Kisha nikafikiri: Nitafia kiotani mwangu nimetulia; siku za maisha yangu zitaongezeka kama mchanga. Mimi ni kama mti uliotandaza mizizi majini, umande wa usiku huburudisha matawi yangu. Napata fahari mpya daima, na nguvu zangu tayari kama mshale na upinde. “Wakati huo watu walinisikiliza na kungoja, walikaa kimya kungojea shauri langu. Nilipomaliza kusema hawakuwa na cha kuongeza, maneno yangu yaliwakolea kama matone ya mvua. Watu waliningojea kama wangojeavyo mvua, walikuwa kama watu wanaotazamia msimu wa vuli. Walipokata tamaa niliwaonesha uso wa furaha, uchangamfu wa uso wangu wakaungangania. Niliwatangulia kuwaongoza, nikawaonesha njia; nilikuwa kwao kama mfalme kati ya majeshi yake; kama mtu anayewafariji wenye msiba.