Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yohane 6:32-59

Yohane 6:32-59 BHN

Yesu akawaambia, “Kweli nawaambieni, Mose hakuwapeni mkate kutoka mbinguni; Baba yangu ndiye awapaye nyinyi mkate wa kweli kutoka mbinguni. Maana mkate wa Mungu ni yule ashukaye kutoka mbinguni na aupaye ulimwengu uhai.” Basi, wakamwambia, “Bwana, tupe daima mkate huo.” Yesu akawaambia, “Mimi ndimi mkate wa uhai. Anayekuja kwangu hataona njaa; anayeniamini hataona kiu kamwe. Lakini niliwaambieni kwamba ingawa mmeniona hamniamini. Wote anaonipa Baba watakuja kwangu; nami kamwe sitamtupa nje yeyote anayekuja kwangu, kwani nimeshuka kutoka mbinguni si kwa ajili ya kufanya matakwa yangu, ila kutimiza matakwa ya yule aliyenituma. Na matakwa ya yule aliyenituma ndiyo haya: Nisimpoteze hata mmoja kati ya wale alionipa, ila niwafufue wote siku ya mwisho. Maana anachotaka Baba yangu ndicho hiki: Kila amwonaye Mwana na kumwamini awe na uhai wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho.” Basi, Wayahudi wakaanza kunungunika kwa kuwa alisema: “Mimi ni mkate ulioshuka kutoka mbinguni.” Wakasema, “Je, huyu si mwana wa Yosefu? Tunamjua baba yake na mama yake! Basi, anawezaje kusema kwamba ameshuka kutoka mbinguni?” Yesu akawaambia, “Acheni kunungunika nyinyi kwa nyinyi. Hakuna mtu awezaye kuja kwangu, Baba aliyenituma asipomvuta kwangu; nami nitamfufua mtu huyo siku ya mwisho. Manabii wameandika: ‘Watu wote watafundishwa na Mungu.’ Kila mtu anayemsikia Baba na kujifunza kutoka kwake, huja kwangu. Hii haina maana kwamba yupo mtu aliyemwona Baba, isipokuwa yule aliyetoka kwa Mungu; huyo ndiye aliyemwona Baba. Kweli, nawaambieni, anayeamini anao uhai wa milele. Mimi ni mkate wa uhai. Wazee wenu walikula mana kule jangwani, lakini walikufa. Lakini huu ni mkate unaoshuka kutoka mbinguni ili yeyote atakayeula asife. Mimi ni mkate hai ulioshuka kutoka mbinguni. Mtu yeyote akila mkate huu ataishi milele. Na mkate nitakaompa ni mwili wangu ninaoutoa kwa ajili ya uhai wa ulimwengu.” Ndipo Wayahudi wakaanza kubishana kati yao: “Anawezaje huyu kutupa mwili wake, tule?” Yesu akawaambia, “Kweli nawaambieni, msipokula mwili wa Mwana wa Mtu na kunywa damu yake, hamtakuwa na uhai ndani yenu. Anayekula mwili wangu na kunywa damu yangu anao uhai wa milele, nami nitamfufua siku ya mwisho. Maana mwili wangu ni chakula cha kweli, na damu yangu ni kinywaji cha kweli. Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu, akaa ndani yangu, nami nakaa ndani yake. Baba aliye hai alinituma, nami naishi kwa sababu yake; vivyo hivyo anilaye mimi ataishi pia kwa sababu yangu. Basi, huu ndio mkate ulioshuka kutoka mbinguni; si kama mana waliyokula babu zenu, wakafa. Aulaye mkate huu atakuwa hai milele.” Yesu alisema hayo alipokuwa akifundisha katika sunagogi kule Kafarnaumu.

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Yohane 6:32-59

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha