Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yn 6:32-59

Yn 6:32-59 SUV

Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambieni, Siye Musa aliyewapa chakula kile cha mbinguni, bali Baba yangu anawapa ninyi chakula cha kweli kitokacho mbinguni. Kwa maana chakula cha Mungu ni kile kishukacho kutoka mbinguni na kuupa ulimwengu uzima. Basi wakamwambia, Bwana, sikuzote utupe chakula hiki. Yesu akawaambia, Mimi ndimi chakula cha uzima; yeye ajaye kwangu hataona njaa kabisa, naye aniaminiye hataona kiu kamwe. Lakini naliwaambia ya kwamba mmeniona wala hamwamini. Wote anipao Baba watakuja kwangu; wala ye yote ajaye kwangu sitamtupa nje kamwe. Kwa kuwa mimi sikushuka kutoka mbinguni ili niyafanye mapenzi yangu, bali mapenzi yake aliyenipeleka. Na mapenzi yake aliyenipeleka ni haya, ya kwamba katika wote alionipa nisimpoteze hata mmoja, bali nimfufue siku ya mwisho. Kwa kuwa mapenzi yake Baba yangu ni haya, ya kwamba kila amtazamaye Mwana na kumwamini yeye, awe na uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho. Basi Wayahudi wakamnung’unikia, kwa sababu alisema, Mimi ni chakula kilichoshuka kutoka mbinguni. Wakasema, Je! Huyu siye Yesu, mwana wa Yusufu, ambaye twamjua babaye na mamaye? Sasa asemaje huyu, Nimeshuka kutoka mbinguni? Basi Yesu akajibu, akawaambia, Msinung’unike ninyi kwa ninyi. Hakuna mtu awezaye kuja kwangu, asipovutwa na Baba aliyenipeleka; nami nitamfufua siku ya mwisho. Imeandikwa katika manabii, Na wote watakuwa wamefundishwa na Mungu. Basi kila aliyesikia na kujifunza kwa Baba huja kwangu. Si kwamba mtu amemwona Baba, ila yeye atokaye kwa Mungu; huyo ndiye aliyemwona Baba. Amin, amin, nawaambia, Yeye aaminiye yuna uzima wa milele. Mimi ndimi chakula cha uzima. Baba zenu waliila mana jangwani; wakafa. Hiki ni chakula kishukacho kutoka mbinguni, kwamba mtu akile wala asife. Mimi ndimi chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni; mtu akila chakula hiki, ataishi milele. Na chakula nitakachotoa mimi ni mwili wangu, kwa ajili ya uzima wa ulimwengu. Basi Wayahudi walishindana wao kwa wao wakisema, Awezaje mtu huyu kutupa sisi mwili wake ili tuule? Basi Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambieni, Msipoula mwili wake Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake, hamna uzima ndani yenu. Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho. Kwa maana mwili wangu ni chakula cha kweli, na damu yangu ni kinywaji cha kweli. Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake. Kama vile Baba aliye hai alivyonituma mimi, nami ni hai kwa Baba; kadhalika naye mwenye kunila atakuwa hai kwa mimi. Hiki ndicho chakula kishukacho kutoka mbinguni; si kama mababa walivyokula, wakafa; bali akilaye chakula hicho ataishi milele. Maneno hayo aliyasema katika sinagogi, alipokuwa akifundisha, huko Kapernaumu.

Soma Yn 6

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Yn 6:32-59

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha