Yohane 18:1-14
Yohane 18:1-14 BHN
Yesu alipokwisha sema hayo, alikwenda ngambo ya kijito Kedroni, pamoja na wanafunzi wake. Mahali hapo palikuwa na bustani, naye Yesu akaingia humo pamoja na wanafunzi wake. Yuda, aliyemsaliti Yesu, alipajua mahali hapo kwani mara nyingi Yesu alikutana na wanafunzi wake huko. Basi, Yuda alichukua kikosi cha askari na walinzi kutoka kwa makuhani wakuu na Mafarisayo, akaja nao bustanini wakiwa na taa, mienge na silaha. Yesu, hali akijua yote yatakayompata, akatokea, akawauliza, “Mnamtafuta nani?” Nao wakamjibu, “Yesu Mnazareti!” Yesu akawaambia, “Mimi ndiye.” Msaliti Yuda alikuwa amesimama hapo pamoja nao. Basi, Yesu alipowaambia: “Mimi ndiye,” wakarudi nyuma, wakaanguka chini. Yesu akawauliza tena, “Mnamtafuta nani?” Wakamjibu, “Yesu Mnazareti!” Yesu akawaambia, “Nimekwisha waambieni kwamba mimi ndiye. Basi, kama mnanitafuta mimi, waacheni hawa waende zao.” ( Alisema hayo ili yapate kutimia yale aliyosema: “Wale ulionipa sikumpoteza hata mmoja.”) Simoni Petro alikuwa na upanga; basi, akauchomoa, akamkata sikio la kulia mtumishi wa kuhani mkuu. Mtumishi huyo aliitwa Malko. Basi, Yesu akamwambia Petro, “Rudisha upanga wako alani. Je, nisinywe kikombe cha mateso alichonipa Baba?” Kile kikosi cha askari, mkuu wake na walinzi wa Wayahudi walimkamata Yesu, wakamfunga na kumpeleka kwanza kwa Anasi; Anasi alikuwa baba mkwe wa Kayafa ambaye alikuwa kuhani mkuu mwaka huo. Huyo Kayafa ndiye aliyekuwa amewashauri Wayahudi kwamba ni afadhali mtu mmoja afe kwa ajili ya watu.