Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yohane 18:1-14

Yohane 18:1-14 Biblia Habari Njema (BHN)

Yesu alipokwisha sema hayo, alikwenda ngambo ya kijito Kedroni, pamoja na wanafunzi wake. Mahali hapo palikuwa na bustani, naye Yesu akaingia humo pamoja na wanafunzi wake. Yuda, aliyemsaliti Yesu, alipajua mahali hapo kwani mara nyingi Yesu alikutana na wanafunzi wake huko. Basi, Yuda alichukua kikosi cha askari na walinzi kutoka kwa makuhani wakuu na Mafarisayo, akaja nao bustanini wakiwa na taa, mienge na silaha. Yesu, hali akijua yote yatakayompata, akatokea, akawauliza, “Mnamtafuta nani?” Nao wakamjibu, “Yesu Mnazareti!” Yesu akawaambia, “Mimi ndiye.” Msaliti Yuda alikuwa amesimama hapo pamoja nao. Basi, Yesu alipowaambia: “Mimi ndiye,” wakarudi nyuma, wakaanguka chini. Yesu akawauliza tena, “Mnamtafuta nani?” Wakamjibu, “Yesu Mnazareti!” Yesu akawaambia, “Nimekwisha waambieni kwamba mimi ndiye. Basi, kama mnanitafuta mimi, waacheni hawa waende zao.” ( Alisema hayo ili yapate kutimia yale aliyosema: “Wale ulionipa sikumpoteza hata mmoja.”) Simoni Petro alikuwa na upanga; basi, akauchomoa, akamkata sikio la kulia mtumishi wa kuhani mkuu. Mtumishi huyo aliitwa Malko. Basi, Yesu akamwambia Petro, “Rudisha upanga wako alani. Je, nisinywe kikombe cha mateso alichonipa Baba?” Kile kikosi cha askari, mkuu wake na walinzi wa Wayahudi walimkamata Yesu, wakamfunga na kumpeleka kwanza kwa Anasi; Anasi alikuwa baba mkwe wa Kayafa ambaye alikuwa kuhani mkuu mwaka huo. Huyo Kayafa ndiye aliyekuwa amewashauri Wayahudi kwamba ni afadhali mtu mmoja afe kwa ajili ya watu.

Shirikisha
Soma Yohane 18

Yohane 18:1-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Alipokwisha kusema hayo, Yesu alitoka pamoja na wanafunzi wake kwenda ng'ambo ya kijito Kedroni, palipokuwapo bustani; akaingia yeye na wanafunzi wake. Naye Yuda, yule aliyetaka kumsaliti, alipajua mahali pale; kwa sababu Yesu alikuwa akienda huko mara nyingi pamoja na wanafunzi wake. Basi Yuda, akiisha kupokea kikosi cha askari na watumishi waliotoka kwa wakuu wa makuhani na Mafarisayo, akaenda huko na taa na mienge na silaha. Basi Yesu, huku akijua yote yatakayompata, akatokea, akawaambia, Ni nani mnayemtafuta? Wao wakamjibu, Ni Yesu Mnazareti. Yesu akawaambia, Ni mimi. Yuda naye aliyemsaliti alikuwa amesimama pamoja nao. Basi alipowaambia, Ni mimi, walirudi nyuma, wakaanguka chini. Basi akawauliza tena, Mnamtafuta nani? Wakasema, Yesu Mnazareti. Yesu akajibu, Nimekwisha kuwaambieni ya kwamba ni mimi; basi ikiwa mnanitafuta mimi, waacheni hawa waende zao. Ili litimizwe lile neno alilolisema, Wale ulionipa sikumpoteza hata mmoja wao. Basi Simoni Petro alikuwa na upanga, akaufuta, akampiga mtumwa wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio la kulia. Na yule mtumwa jina lake ni Malko. Basi Yesu akamwambia Petro, Rudisha upanga alani mwake; je! Kikombe alichonipa Baba, mimi nisikinywee? Basi wale askari na yule jemadari na wale watumishi wa Wayahudi walimkamata Yesu, wakamfunga. Wakampeleka kwa Anasi kwanza; maana alikuwa baba mkwe wa Kayafa, yule aliyekuwa Kuhani Mkuu mwaka ule. Naye Kayafa ndiye yule aliyewapa Wayahudi lile shauri ya kwamba yafaa mtu mmoja afe kwa ajili ya watu.

Shirikisha
Soma Yohane 18

Yohane 18:1-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Alipokwisha kusema hayo, Yesu alitoka pamoja na wanafunzi wake kwenda ng’ambo ya kijito Kedroni, palipokuwapo bustani; akaingia yeye na wanafunzi wake. Naye Yuda, yule aliyetaka kumsaliti, alipajua mahali pale; kwa sababu Yesu alikuwa akienda huko mara nyingi pamoja na wanafunzi wake. Basi Yuda, akiisha kupokea kikosi cha askari na watumishi waliotoka kwa wakuu wa makuhani na Mafarisayo, akaenda huko na taa na mienge na silaha. Basi Yesu, hali akijua yote yatakayompata, akatokea, akawaambia, Ni nani mnayemtafuta? Wao wakamjibu, Ni Yesu Mnazareti. Yesu akawaambia, Ni mimi. Yuda naye aliyemsaliti alikuwa amesimama pamoja nao. Basi alipowaambia, Ni mimi, walirudi nyuma, wakaanguka chini. Basi akawauliza tena, Mnamtafuta nani? Wakasema, Yesu Mnazareti. Yesu akajibu, Nimekwisha kuwaambieni ya kwamba ni mimi; basi ikiwa mnanitafuta mimi, waacheni hawa waende zao. Ili litimizwe lile neno alilolisema, Wale ulionipa sikumpoteza hata mmoja wao. Basi Simoni Petro alikuwa na upanga, akaufuta, akampiga mtumwa wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio la kuume. Na yule mtumwa jina lake ni Malko. Basi Yesu akamwambia Petro, Rudisha upanga alani mwake; je! Kikombe alichonipa Baba, mimi nisikinywee? Basi wale askari na yule jemadari na wale watumishi wa Wayahudi walimkamata Yesu, wakamfunga. Wakamchukua kwa Anasi kwanza; maana alikuwa mkwewe Kayafa, yule aliyekuwa Kuhani Mkuu mwaka ule. Naye Kayafa ndiye yule aliyewapa Wayahudi lile shauri ya kwamba yafaa mtu mmoja afe kwa ajili ya watu.

Shirikisha
Soma Yohane 18

Yohane 18:1-14 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Yesu alipomaliza kuomba, akaondoka na wanafunzi wake wakavuka Bonde la Kidroni. Upande wa pili palikuwa na bustani, yeye na wanafunzi wake wakaingia humo. Basi Yuda, yule aliyemsaliti alipafahamu mahali hapo kwani Yesu alikuwa akikutana humo na wanafunzi wake mara kwa mara. Hivyo Yuda akaja bustanini. Aliongoza kikosi cha askari wa Kirumi, na baadhi ya maafisa kutoka kwa viongozi wa makuhani na Mafarisayo. Nao walikuwa wamechukua taa, mienge na silaha. Yesu akijua yale yote yatakayompata, akajitokeza mbele yao akawauliza, “Mnamtafuta nani?” Wao wakamjibu, “Yesu wa Nazareti.” Yesu akawajibu, “Mimi ndiye.” Yuda, yule aliyemsaliti alikuwa amesimama pamoja nao. Yesu alipowaambia, “Mimi ndiye,” walirudi nyuma na kuanguka chini! Akawauliza tena, “Mnamtafuta nani?” Nao wakamjibu, “Yesu wa Nazareti.” Yesu akawaambia, “Nimekwisha kuwaambia kuwa, mimi ndiye; kwa hiyo kama mnanitafuta mimi, waacheni hawa watu waende zao.” Hii ilikuwa ili litimie lile neno alilosema, “Sikumpoteza hata mmoja miongoni mwa wale ulionipa.” Simoni Petro, aliyekuwa na upanga, akaufuta na kumkata sikio la kuume mtumishi wa kuhani mkuu. Jina la mtumishi huyo aliitwa Malko. Yesu akamwambia Petro, “Rudisha upanga wako kwenye ala yake. Je, hainipasi kukinywea kikombe alichonipa Baba?” Hivyo wale askari, wakiwa pamoja na majemadari wao na maafisa wa Wayahudi, wakamkamata Yesu na kumfunga. Kwanza wakampeleka kwa Anasi, mkwewe Kayafa, aliyekuwa kuhani mkuu mwaka ule. Kayafa ndiye alikuwa amewashauri Wayahudi kwamba imempasa mtu mmoja kufa kwa ajili ya watu.

Shirikisha
Soma Yohane 18