Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yohane 12:20-50

Yohane 12:20-50 BHN

Kulikuwa na Wagiriki kadhaa miongoni mwa watu waliokuwa wamefika Yerusalemu kuabudu wakati wa sikukuu hiyo. Hao walimwendea Filipo, mwenyeji wa Bethsaida katika Galilaya, wakasema, “Mheshimiwa, tunataka kumwona Yesu.” Filipo akaenda, akamwambia Andrea, nao wawili wakaenda kumwambia Yesu. Yesu akawaambia, “Saa ya kutukuzwa kwa Mwana wa Mtu imefika! Kweli nawaambieni, punje ya ngano hubaki punje tu isipokuwa ikianguka katika udongo na kufa. Kama ikifa, basi huzaa matunda mengi. Anayependa maisha yake, atayapoteza; anayeyachukia maisha yake katika ulimwengu huu, atayaweka kwa ajili ya uhai wa milele. Anayetaka kunitumikia ni lazima anifuate, hivyo kwamba popote pale nilipo mimi ndipo na mtumishi wangu atakapokuwa. Mtu yeyote anayenitumikia Baba yangu atampa heshima. “Sasa roho yangu imefadhaika, na niseme nini? Je, niseme: ‘Baba, usiruhusu saa hii inifikie?’ Lakini ndiyo maana nimekuja – ili nipite katika saa hii. Baba, ulitukuze jina lako.” Hapo sauti ikasema kutoka mbinguni, “Nimelitukuza, na nitalitukuza tena.” Umati wa watu waliokuwa wamesimama hapo walisikia sauti hiyo, na baadhi yao walisema, “Ni ngurumo.” Lakini wengine wakasema, “Malaika ameongea naye!” Lakini Yesu akawaambia, “Sauti hiyo haikutokea kwa ajili yangu mimi, ila kwa ajili yenu. Sasa ndio wakati wa ulimwengu huu kuhukumiwa; sasa mtawala wa ulimwengu huu atapinduliwa. Nami nitakapoinuliwa juu ya nchi nitamvuta kila mmoja kwangu.” (Kwa kusema hivyo alionesha atakufa kifo gani). Basi, umati huo ukamjibu, “Sisi tunaambiwa na sheria yetu kwamba Kristo atadumu milele. Wawezaje basi, kusema ati Mwana wa Mtu anapaswa kuinuliwa? Huyo Mwana wa Mtu ni nani?” Yesu akawaambia, “Mwanga bado uko nanyi kwa muda mfupi. Tembeeni mngali mnao huo mwanga ili giza lisiwapate; maana atembeaye gizani hajui aendako. Basi, wakati mnao huo mwanga uaminini ili mpate kuwa watu wa mwanga.” Baada ya kusema maneno hayo, Yesu alikwenda zake na kujificha mbali nao. Ingawa Yesu alifanya miujiza hii yote mbele yao, wao hawakumwamini. Hivyo maneno aliyosema nabii Isaya yakatimia: “Bwana, nani aliyeuamini ujumbe wetu? Na uwezo wa Bwana umedhihirishwa kwa nani?” Hivyo hawakuweza kuamini, kwani Isaya alisema tena: “Mungu ameyapofusha macho yao, amezipumbaza akili zao; wasione kwa macho yao, wasielewe kwa akili zao; wala wasinigeukie, asema Bwana, ili nipate kuwaponya.” Isaya alisema maneno haya kwa sababu aliuona utukufu wa Yesu, akasema habari zake. Hata hivyo, wengi wa viongozi wa Wayahudi walimwamini Yesu. Lakini kwa sababu ya Mafarisayo, hawakumkiri hadharani kwa kuogopa kwamba watatengwa na sunagogi. Walipendelea kusifiwa na watu kuliko kusifiwa na Mungu. Kisha Yesu akasema kwa sauti kubwa, “Mtu anayeniamini, haniamini mimi tu, ila anamwamini pia yule aliyenituma. Anayeniona mimi anamwona pia yule aliyenituma. Mimi ni mwanga, nami nimekuja ulimwenguni ili wote wanaoniamini wasibaki gizani. Anayeyasikia maneno yangu lakini hayashiki, mimi sitamhukumu; maana sikuja kuuhukumu ulimwengu bali kuuokoa. Asiyeyashika maneno yangu anaye wa kumhukumu: Neno lile nililosema ni hakimu wake siku ya mwisho. Mimi sikunena kwa mamlaka yangu mwenyewe, ila Baba aliyenituma ndiye aliyeniamuru niseme nini na niongee nini. Nami najua kuwa amri yake huleta uhai wa milele. Basi, mimi nasema tu yale Baba aliyoniagiza niyaseme.”