Yohane 12:20-50
Yohane 12:20-50 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Palikuwa na Wagiriki kadhaa miongoni mwa watu waliokwea kwenda kuabudu kwenye sikukuu. Basi hao walimwendea Filipo, mtu wa Bethsaida ya Galilaya, wakamwomba, wakisema, Bwana, sisi tunataka kumwona Yesu. Filipo akaenda, akamwambia Andrea; kisha Andrea na Filipo wakamwambia Yesu. Naye Yesu akawajibu, akasema, Saa imefika atukuzwe Mwana wa Adamu. Amin, amin, nawaambia, Chembe ya ngano isipoanguka katika nchi, ikafa, hukaa hali iyo hiyo peke yake; bali ikifa, hutoa mazao mengi. Yeye aipendaye nafsi yake ataiangamiza; naye aichukiaye nafsi yake katika ulimwengu huu ataisalimisha hata uzima wa milele. Mtu akinitumikia, na anifuate; nami nilipo, ndipo na mtumishi wangu atakapokuwapo. Tena mtu akinitumikia, Baba atamheshimu. Sasa roho yangu imefadhaika; nami nisemeje? Baba, uniokoe katika saa hii? Lakini ni kwa ajili ya hayo nilivyoifikia saa hii. Baba, ulitukuze jina lako. Basi ikaja sauti kutoka mbinguni, Nimelitukuza, nami nitalitukuza tena. Basi mkutano uliosimama karibu wakasikia, walisema ya kwamba kumekuwa ngurumo; wengine walisema, Malaika amesema naye. Yesu akajibu, akasema, Sauti hiyo haikuwako kwa ajili yangu, bali kwa ajili yenu. Sasa hukumu ya ulimwengu huu ipo; sasa mkuu wa ulimwengu huu atatupwa nje. Nami nikiinuliwa juu ya nchi, nitawavuta wote kwangu. Aliyanena hayo akionesha ni mauti gani atakayokufa. Basi mkutano wakamjibu, Sisi tumesikia katika torati ya kwamba Kristo adumu hata milele; nawe wasemaje ya kwamba imempasa Mwana wa Adamu kuinuliwa? Huyu Mwana wa Adamu ni nani? Basi Yesu akawaambia, Nuru ingaliko pamoja nanyi muda kidogo. Nendeni maadamu mnayo nuru hiyo, giza lisije likawaweza; maana aendaye gizani hajui aendako. Maadamu mnayo nuru, iaminini nuru hiyo, ili mpate kuwa wana wa nuru. Hayo aliyasema Yesu, akaenda zake, akajificha wasimwone. Lakini ingawa amefanya ishara nyingi namna hiyo mbele yao, hawakumwamini; ili litimie lile neno la nabii Isaya alilolisema, Bwana, ni nani aliyezisadiki habari zetu; Na mkono wa Bwana amefunuliwa nani? Ndiyo sababu wao hawakuweza kusadiki; kwa maana Isaya alisema tena, Amewapofusha macho, Ameifanya mizito mioyo yao; Wasije wakaona kwa macho yao, Wakafahamu kwa mioyo yao, Wakaongoka, nikawaponya. Maneno hayo aliyasema Isaya, kwa kuwa aliuona utukufu wake, akataja habari zake. Lakini hata katika wakuu walikuwamo wengi waliomwamini; lakini kwa sababu ya Mafarisayo hawakumkiri, wasije wakatengwa na sinagogi. Kwa maana walipenda utukufu wa wanadamu kuliko utukufu wa Mungu. Naye Yesu akapaza sauti, akasema, Yeye aniaminiye mimi, haniamini mimi bali yeye aliyenituma. Naye anitazamaye mimi amtazama yeye aliyenituma. Mimi nimekuja ili niwe nuru ya ulimwengu, ili kila mtu aniaminiye mimi asikae gizani. Na mtu akiyasikia maneno yangu, asiyashike, mimi simhukumu; maana sikuja ili niuhukumu ulimwengu, ila niuokoe ulimwengu. Yeye anikataaye mimi, asiyeyakubali maneno yangu, anaye amhukumuye; neno hilo nililolinena ndilo litakalomhukumu siku ya mwisho. Kwa sababu mimi sikunena kwa nafsi yangu tu; bali Baba aliyenituma, yeye mwenyewe ameniagiza nitakayonena na nitakayosema. Nami najua ya kuwa agizo lake ni uzima wa milele; basi hayo ninenayo mimi, kama Baba alivyoniambia, ndivyo ninenavyo.
Yohane 12:20-50 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Palikuwa na Wayunani kadha wa kadha miongoni mwa watu waliokwea kwenda kuabudu kwenye sikukuu. Basi hao walimwendea Filipo, mtu wa Bethsaida ya Galilaya, wakamwomba, wakisema, Bwana, sisi tunataka kumwona Yesu. Filipo akaenda, akamwambia Andrea; kisha Andrea na Filipo wakamwambia Yesu. Naye Yesu akawajibu, akasema, Saa imefika atukuzwe Mwana wa Adamu. Amin, amin, nawaambia, Chembe ya ngano isipoanguka katika nchi, ikafa, hukaa hali iyo hiyo peke yake; bali ikifa, hutoa mazao mengi. Yeye aipendaye nafsi yake ataiangamiza; naye aichukiaye nafsi yake katika ulimwengu huu ataisalimisha hata uzima wa milele. Mtu akinitumikia, na anifuate; nami nilipo, ndipo na mtumishi wangu atakapokuwapo. Tena mtu akinitumikia, Baba atamheshimu. Sasa roho yangu imefadhaika; nami nisemeje? Baba, uniokoe katika saa hii? Lakini ni kwa ajili ya hayo nilivyoifikia saa hii. Baba, ulitukuze jina lako. Basi ikaja sauti kutoka mbinguni, Nimelitukuza, nami nitalitukuza tena. Basi mkutano uliosimama karibu wakasikia, walisema ya kwamba kumekuwa ngurumo; wengine walisema, Malaika amesema naye. Yesu akajibu, akasema, Sauti hiyo haikuwako kwa ajili yangu, bali kwa ajili yenu. Sasa hukumu ya ulimwengu huu ipo; sasa mkuu wa ulimwengu huu atatupwa nje. Nami nikiinuliwa juu ya nchi, nitawavuta wote kwangu. Aliyanena hayo akionyesha ni mauti gani atakayokufa. Basi mkutano wakamjibu, Sisi tumesikia katika torati ya kwamba Kristo adumu hata milele; nawe wasemaje ya kwamba imempasa Mwana wa Adamu kuinuliwa? Huyu Mwana wa Adamu ni nani? Basi Yesu akawaambia, Nuru ingaliko pamoja nanyi muda kidogo. Enendeni maadamu mnayo nuru hiyo, giza lisije likawaweza; maana aendaye gizani hajui aendako. Maadamu mnayo nuru, iaminini nuru hiyo, ili mpate kuwa wana wa nuru. Hayo aliyasema Yesu, akaenda zake, akajificha wasimwone. Walakini ajapokuwa amefanya ishara nyingi namna hiyo mbele yao, hawakumwamini; ili litimie lile neno la nabii Isaya alilolisema, Bwana, ni nani aliyezisadiki habari zetu; Na mkono wa Bwana amefunuliwa nani? Ndiyo sababu wao hawakuweza kusadiki; kwa maana Isaya alisema tena, Amewapofusha macho, Ameifanya mizito mioyo yao; Wasije wakaona kwa macho yao, Wakafahamu kwa mioyo yao, Wakaongoka, nikawaponya. Maneno hayo aliyasema Isaya, kwa kuwa aliuona utukufu wake, akataja habari zake. Walakini hata katika wakuu walikuwamo wengi waliomwamini; lakini kwa sababu ya Mafarisayo hawakumkiri, wasije wakatengwa na sinagogi. Kwa maana walipenda utukufu wa wanadamu kuliko utukufu wa Mungu. Naye Yesu akapaza sauti, akasema, Yeye aniaminiye mimi, haniamini mimi bali yeye aliyenipeleka. Naye anitazamaye mimi amtazama yeye aliyenipeleka. Mimi nimekuja ili niwe nuru ya ulimwengu, ili kila mtu aniaminiye mimi asikae gizani. Na mtu akiyasikia maneno yangu, asiyashike, mimi simhukumu; maana sikuja ili niuhukumu ulimwengu, ila niuokoe ulimwengu. Yeye anikataaye mimi, asiyeyakubali maneno yangu, anaye amhukumuye; neno hilo nililolinena ndilo litakalomhukumu siku ya mwisho. Kwa sababu mimi sikunena kwa nafsi yangu tu; bali Baba aliyenipeleka, yeye mwenyewe ameniagiza nitakayonena na nitakayosema. Nami najua ya kuwa agizo lake ni uzima wa milele; basi hayo ninenayo mimi, kama Baba alivyoniambia, ndivyo ninenavyo.
Yohane 12:20-50 Biblia Habari Njema (BHN)
Kulikuwa na Wagiriki kadhaa miongoni mwa watu waliokuwa wamefika Yerusalemu kuabudu wakati wa sikukuu hiyo. Hao walimwendea Filipo, mwenyeji wa Bethsaida katika Galilaya, wakasema, “Mheshimiwa, tunataka kumwona Yesu.” Filipo akaenda, akamwambia Andrea, nao wawili wakaenda kumwambia Yesu. Yesu akawaambia, “Saa ya kutukuzwa kwa Mwana wa Mtu imefika! Kweli nawaambieni, punje ya ngano hubaki punje tu isipokuwa ikianguka katika udongo na kufa. Kama ikifa, basi huzaa matunda mengi. Anayependa maisha yake, atayapoteza; anayeyachukia maisha yake katika ulimwengu huu, atayaweka kwa ajili ya uhai wa milele. Anayetaka kunitumikia ni lazima anifuate, hivyo kwamba popote pale nilipo mimi ndipo na mtumishi wangu atakapokuwa. Mtu yeyote anayenitumikia Baba yangu atampa heshima. “Sasa roho yangu imefadhaika, na niseme nini? Je, niseme: ‘Baba, usiruhusu saa hii inifikie?’ Lakini ndiyo maana nimekuja – ili nipite katika saa hii. Baba, ulitukuze jina lako.” Hapo sauti ikasema kutoka mbinguni, “Nimelitukuza, na nitalitukuza tena.” Umati wa watu waliokuwa wamesimama hapo walisikia sauti hiyo, na baadhi yao walisema, “Ni ngurumo.” Lakini wengine wakasema, “Malaika ameongea naye!” Lakini Yesu akawaambia, “Sauti hiyo haikutokea kwa ajili yangu mimi, ila kwa ajili yenu. Sasa ndio wakati wa ulimwengu huu kuhukumiwa; sasa mtawala wa ulimwengu huu atapinduliwa. Nami nitakapoinuliwa juu ya nchi nitamvuta kila mmoja kwangu.” (Kwa kusema hivyo alionesha atakufa kifo gani). Basi, umati huo ukamjibu, “Sisi tunaambiwa na sheria yetu kwamba Kristo atadumu milele. Wawezaje basi, kusema ati Mwana wa Mtu anapaswa kuinuliwa? Huyo Mwana wa Mtu ni nani?” Yesu akawaambia, “Mwanga bado uko nanyi kwa muda mfupi. Tembeeni mngali mnao huo mwanga ili giza lisiwapate; maana atembeaye gizani hajui aendako. Basi, wakati mnao huo mwanga uaminini ili mpate kuwa watu wa mwanga.” Baada ya kusema maneno hayo, Yesu alikwenda zake na kujificha mbali nao. Ingawa Yesu alifanya miujiza hii yote mbele yao, wao hawakumwamini. Hivyo maneno aliyosema nabii Isaya yakatimia: “Bwana, nani aliyeuamini ujumbe wetu? Na uwezo wa Bwana umedhihirishwa kwa nani?” Hivyo hawakuweza kuamini, kwani Isaya alisema tena: “Mungu ameyapofusha macho yao, amezipumbaza akili zao; wasione kwa macho yao, wasielewe kwa akili zao; wala wasinigeukie, asema Bwana, ili nipate kuwaponya.” Isaya alisema maneno haya kwa sababu aliuona utukufu wa Yesu, akasema habari zake. Hata hivyo, wengi wa viongozi wa Wayahudi walimwamini Yesu. Lakini kwa sababu ya Mafarisayo, hawakumkiri hadharani kwa kuogopa kwamba watatengwa na sunagogi. Walipendelea kusifiwa na watu kuliko kusifiwa na Mungu. Kisha Yesu akasema kwa sauti kubwa, “Mtu anayeniamini, haniamini mimi tu, ila anamwamini pia yule aliyenituma. Anayeniona mimi anamwona pia yule aliyenituma. Mimi ni mwanga, nami nimekuja ulimwenguni ili wote wanaoniamini wasibaki gizani. Anayeyasikia maneno yangu lakini hayashiki, mimi sitamhukumu; maana sikuja kuuhukumu ulimwengu bali kuuokoa. Asiyeyashika maneno yangu anaye wa kumhukumu: Neno lile nililosema ni hakimu wake siku ya mwisho. Mimi sikunena kwa mamlaka yangu mwenyewe, ila Baba aliyenituma ndiye aliyeniamuru niseme nini na niongee nini. Nami najua kuwa amri yake huleta uhai wa milele. Basi, mimi nasema tu yale Baba aliyoniagiza niyaseme.”
Yohane 12:20-50 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Basi palikuwa Wayunani fulani miongoni mwa wale waliokuwa wamekwenda kuabudu wakati wa Sikukuu. Hawa wakamjia Filipo, ambaye alikuwa mwenyeji wa Bethsaida huko Galilaya, wakiwa na ombi. Wakamwambia, “Tungependa kumwona Yesu.” Filipo akaenda akamweleza Andrea, nao wote wawili wakamwambia Yesu. Yesu akawajibu, “Saa imewadia ya Mwana wa Adamu kutukuzwa. Amin, amin nawaambia, mbegu ya ngano isipoanguka ardhini na kufa, hubakia kama mbegu peke yake. Lakini ikifa huzaa mbegu nyingi. Mtu yeyote anayependa maisha yake atayapoteza, naye ayachukiaye maisha yake katika ulimwengu huu atayaokoa hata kwa uzima wa milele. Mtu yeyote akinitumikia lazima anifuate, nami mahali nilipo ndipo mtumishi wangu atakapokuwa. Mtu akinitumikia, Baba yangu atamheshimu. “Sasa roho yangu imefadhaika sana. Niseme nini? ‘Baba, niokoe katika saa hii.’ Lakini ni kwa kusudi hili nimeufikia wakati huu. Baba, litukuze jina lako.” Ndipo ikaja sauti kutoka mbinguni, “Nimelitukuza, nami nitalitukuza tena.” Ule umati wa watu uliokuwa mahali pale uliisikia nao ukasema, “Hiyo ni sauti ya radi,” wengine wakasema, “Malaika ameongea naye.” Yesu akawaambia, “Sauti hii imesikika kwa faida yenu, wala si kwa faida yangu. Sasa ni saa ya hukumu kwa ajili ya ulimwengu huu, sasa mkuu wa ulimwengu huu atatupwa nje. Lakini mimi, nikiinuliwa kutoka nchi, nitawavuta watu wote waje kwangu.” Yesu aliyasema haya akionyesha ni kifo gani atakachokufa. Ule umati wa watu ukapiga kelele ukasema, “Tumesikia kutoka Sheria kwamba ‘Kristo adumu milele,’ wewe wawezaje kusema, ‘Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa juu’? Huyu ‘Mwana wa Adamu’ ni nani?” Ndipo Yesu akawaambia, “Bado kitambo kidogo nuru ingalipo pamoja nanyi. Enendeni maadamu mna nuru, msije mkakumbwa na giza. Mtu anayetembea gizani hajui anakokwenda. Wekeni tumaini lenu katika nuru hiyo ili mpate kuwa wana wa nuru.” Baada ya kusema haya, Yesu aliondoka, akajificha wasimwone. Hata baada ya Yesu kufanya miujiza hii yote mbele yao, bado hawakumwamini. Hili lilikuwa ili kutimiza lile neno la nabii Isaya lililosema: “Bwana, ni nani aliyeamini ujumbe wetu, na mkono wa Bwana umefunuliwa kwa nani?” Kwa hivyo hawakuamini, kwa sababu Isaya anasema mahali pengine: “Amewafanya vipofu, na kuifanya mioyo yao kuwa migumu, ili wasiweze kuona kwa macho yao, wala kuelewa kwa mioyo yao, wasije wakageuka nami nikawaponya.” Isaya alisema haya alipoona utukufu wa Yesu na kunena habari zake. Lakini wengi miongoni mwa viongozi wa Wayahudi walimwamini, lakini kwa sababu ya Mafarisayo hawakukiri waziwazi kwa maana waliogopa kufukuzwa katika masinagogi. Wao walipenda sifa za wanadamu kuliko sifa zitokazo kwa Mungu. Yesu akapaza sauti akasema, “Yeyote aniaminiye, haniamini mimi peke yangu, bali yeye aliyenituma. Yeyote anionaye mimi, amemwona yeye aliyenituma. Mimi nimekuja kama nuru ulimwenguni, ili kwamba kila mtu aniaminiye asibaki gizani. “Mimi simhukumu mtu yeyote anayesikia maneno yangu na asiyatii, kwa maana sikuja kuuhukumu ulimwengu, bali kuuokoa. Yuko amhukumuye yeye anikataaye mimi na kutokuyapokea maneno yangu, yaani, yale maneno niliyosema yenyewe yatamhukumu siku ya mwisho. Kwa maana sisemi kwa ajili yangu mwenyewe, bali Baba aliyenituma aliniamuru ni nini cha kusema na jinsi ya kukisema. Nami ninajua amri zake huongoza hadi kwenye uzima wa milele. Hivyo lolote nisemalo, ndilo lile Baba aliloniambia niseme.”