Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yohana 12:20-50

Yohana 12:20-50 NENO

Basi palikuwa Wayunani fulani miongoni mwa wale waliokuwa wameenda kuabudu wakati wa Sikukuu. Hawa wakaenda kwa Filipo, aliyekuwa raia wa Bethsaida huko Galilaya, wakiwa na ombi. Wakamwambia, “Tungependa kumwona Yesu.” Filipo akaenda akamweleza Andrea, nao wote wawili wakamwambia Yesu. Yesu akawajibu, “Saa imewadia ya Mwana wa Adamu kutukuzwa. Amin, amin nawaambia, mbegu ya ngano isipoanguka ardhini na kufa, hubakia kama mbegu peke yake. Lakini ikifa, huzaa mbegu nyingi. Mtu yeyote anayependa maisha yake atayapoteza, naye ayachukiaye maisha yake katika ulimwengu huu atayaokoa hata kwa uzima wa milele. Mtu yeyote akinitumikia lazima anifuate, nami mahali nilipo ndipo mtumishi wangu atakapokuwa. Mtu akinitumikia, Baba yangu atamheshimu. “Sasa roho yangu imefadhaika sana. Niseme nini? ‘Baba, niokoe katika saa hii’? Lakini ni kwa kusudi hili nimeufikia wakati huu. Baba, litukuze jina lako.” Ndipo ikaja sauti kutoka mbinguni, ikasema, “Nimelitukuza, nami nitalitukuza tena.” Umati ule wa watu waliokuwa mahali pale waliisikia ile sauti, nao wakasema hiyo ilikuwa sauti ya radi; wengine wakasema malaika ameongea naye. Yesu akawaambia, “Sauti hii imesikika kwa faida yenu, wala si kwa faida yangu. Sasa ni saa ya hukumu kwa ajili ya ulimwengu huu, sasa mkuu wa ulimwengu huu atatupwa nje. Lakini mimi, nikiinuliwa kutoka nchi, nitawavuta watu wote waje kwangu.” Yesu aliyasema haya akionesha ni kifo gani atakachokufa. Umati ule wa watu wakapaza sauti, wakasema, “Tumesikia kutoka Sheria kwamba Kristo adumu milele; hivyo wewe wawezaje kusema, ‘Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa juu’? Huyu ‘Mwana wa Adamu’ ni nani?” Ndipo Yesu akawaambia, “Bado kitambo kidogo nuru ingali pamoja nanyi. Nendeni maadamu mna nuru, msije mkakumbwa na giza. Mtu anayetembea gizani hajui anakoenda. Wekeni tumaini lenu katika nuru hiyo ili mpate kuwa wana wa nuru.” Baada ya kusema haya, Yesu aliondoka, akajificha wasimwone. Hata baada ya Yesu kufanya miujiza hii yote mbele yao, bado hawakumwamini. Hili lilikuwa ili kutimiza lile neno la nabii Isaya lililosema: “Bwana, ni nani aliyeamini ujumbe wetu, na mkono wa Bwana umefunuliwa kwa nani?” Kwa hivyo hawakuamini, kwa sababu Isaya anasema mahali pengine: “Amewafanya vipofu, na kuifanya mioyo yao kuwa migumu, ili wasiweze kuona kwa macho yao, wala kuelewa kwa mioyo yao, wasije wakageuka nami nikawaponya.” Isaya alisema haya alipoona utukufu wa Yesu na kunena habari zake. Lakini wengi miongoni mwa viongozi wa Wayahudi walimwamini, lakini kwa sababu ya Mafarisayo hawakukiri waziwazi kwa maana waliogopa kufukuzwa katika masinagogi. Wao walipenda sifa za wanadamu kuliko sifa zinazotoka kwa Mungu. Yesu akapaza sauti akasema, “Yeyote aniaminiye, haniamini mimi peke yangu, bali pia yeye aliyenituma. Yeyote anionaye mimi amemwona yeye aliyenituma. Mimi nimekuja kama nuru ulimwenguni, ili kila mtu aniaminiye asibaki gizani. “Mimi simhukumu mtu yeyote anayesikia maneno yangu na asiyatii, kwa maana sikuja kuuhukumu ulimwengu, bali kuuokoa. Yuko anayehukumu yule anayenikataa mimi na kuyakataa maneno yangu; yale maneno niliyoyasema yenyewe yatamhukumu siku ya mwisho. Kwa maana sisemi kwa ajili yangu mwenyewe, bali Baba aliyenituma aliniamuru ni nini cha kusema na jinsi ya kukisema. Nami ninajua amri zake huongoza hadi kwenye uzima wa milele. Hivyo lolote nisemalo, ndilo lile Baba aliloniambia niseme.”