Isaya 1:10-17
Isaya 1:10-17 BHN
Sikilizeni neno la Mwenyezi-Mungu enyi watawala waovu kama wa Sodoma! Sikilizeni mafunzo ya Mungu wetu enyi watu waovu kama wa Gomora! Mwenyezi-Mungu asema hivi; “Wingi wa tambiko zenu ni kitu gani kwangu? Nimezichoka sadaka zenu za kondoo wa kuteketezwa na mafuta ya wanyama wenu wanono. Sipendezwi na damu ya fahali, wala ya wanakondoo, wala ya beberu. Mnapokuja mbele yangu kuniabudu nani aliyewataka mkanyagekanyage nyua zangu? Msiniletee tena matoleo yenu yasiyo na maana; ubani ni chukizo kwangu. Acheni kufanya sikukuu za mwezi mpya, Sabato na mikutano mikubwa ya ibada; sikubali ibada zilizochanganyika na dhambi. Sikukuu zenu za mwezi mpya na nyinginezo moyo wangu wazichukia. Zimekuwa mzigo mzito kwangu, nami nimechoka kuzivumilia. “Mnapoinua mikono yenu kuomba nitauficha uso wangu nisiwaone. Hata mkiomba kwa wingi sitawasikia, maana mikono yenu imejaa damu. Jiosheni, jitakaseni; ondoeni uovu wa matendo yenu mbele yangu. Acheni kutenda maovu, jifunzeni kutenda mema. Tendeni haki, ondoeni udhalimu, walindeni yatima, teteeni haki za wajane.”