Isaya 1:10-17
Isaya 1:10-17 Biblia Habari Njema (BHN)
Sikilizeni neno la Mwenyezi-Mungu enyi watawala waovu kama wa Sodoma! Sikilizeni mafunzo ya Mungu wetu enyi watu waovu kama wa Gomora! Mwenyezi-Mungu asema hivi; “Wingi wa tambiko zenu ni kitu gani kwangu? Nimezichoka sadaka zenu za kondoo wa kuteketezwa na mafuta ya wanyama wenu wanono. Sipendezwi na damu ya fahali, wala ya wanakondoo, wala ya beberu. Mnapokuja mbele yangu kuniabudu nani aliyewataka mkanyagekanyage nyua zangu? Msiniletee tena matoleo yenu yasiyo na maana; ubani ni chukizo kwangu. Acheni kufanya sikukuu za mwezi mpya, Sabato na mikutano mikubwa ya ibada; sikubali ibada zilizochanganyika na dhambi. Sikukuu zenu za mwezi mpya na nyinginezo moyo wangu wazichukia. Zimekuwa mzigo mzito kwangu, nami nimechoka kuzivumilia. “Mnapoinua mikono yenu kuomba nitauficha uso wangu nisiwaone. Hata mkiomba kwa wingi sitawasikia, maana mikono yenu imejaa damu. Jiosheni, jitakaseni; ondoeni uovu wa matendo yenu mbele yangu. Acheni kutenda maovu, jifunzeni kutenda mema. Tendeni haki, ondoeni udhalimu, walindeni yatima, teteeni haki za wajane.”
Isaya 1:10-17 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Lisikieni neno la BWANA, enyi waamuzi wa Sodoma; tegeni masikio msikie sheria ya Mungu wetu, enyi watu wa Gomora. Huu wingi wa sadaka zenu mnazonitolea una faida gani? Asema BWANA. Nimejaa mafuta ya kafara za kondoo dume, na mafuta ya wanyama walionona; nami siifurahii damu ya ng'ombe wala ya wana-kondoo wala ya mbuzi dume. Mjapo ili kuonekana mbele zangu, ni nani aliyetaka neno hili mikononi mwenu, kuzikanyaga nyua zangu? Msilete tena matoleo ya ubatili; uvumba ni chukizo kwangu; mwezi mwandamo na sabato, kuita makutano; siyawezi maovu hayo na makutano ya ibada. Sikukuu zenu za mwezi mpya na karamu zenu zilizoamriwa, nafsi yangu yazichukia; mambo hayo yanilemea; nimechoka kuyachukua. Nanyi mkunjuapo mikono yenu, nitaficha macho yangu nisiwaone; naam, mwombapo maombi mengi, sitasikia; mikono yenu imejaa damu. Jiosheni, jitakaseni; ondoeni uovu wa matendo yenu usiwe mbele za macho yangu; acheni kutenda mabaya; jifunzeni kutenda mema; takeni hukumu na haki; wasaidieni walioonewa; mpatieni yatima haki yake; mteteeni mjane.
Isaya 1:10-17 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Lisikieni neno la BWANA, enyi waamuzi wa Sodoma; tegeni masikio msikie sheria ya Mungu wetu, enyi watu wa Gomora. Huu wingi wa sadaka zenu mnazonitolea una faida gani? Asema BWANA. Nimejaa mafuta ya kafara za kondoo waume, na mafuta ya wanyama walionona; nami siifurahii damu ya ng’ombe wala ya wana-kondoo wala ya mbuzi waume. Mjapo ili kuonekana mbele zangu, ni nani aliyetaka neno hili mikononi mwenu, kuzikanyaga nyua zangu? Msilete tena matoleo ya ubatili; uvumba ni chukizo kwangu; mwezi mpya na sabato, kuita makutano; siyawezi maovu hayo na makutano ya ibada. Sikukuu zenu za mwezi mpya na karamu zenu zilizoamriwa, nafsi yangu yazichukia; mambo hayo yanilemea; nimechoka kuyachukua. Nanyi mkunjuapo mikono yenu, nitaficha macho yangu nisiwaone; naam, mwombapo maombi mengi, sitasikia; mikono yenu imejaa damu. Jiosheni, jitakaseni; ondoeni uovu wa matendo yenu usiwe mbele za macho yangu; acheni kutenda mabaya; jifunzeni kutenda mema; takeni hukumu na haki; wasaidieni walioonewa; mpatieni yatima haki yake; mteteeni mjane.
Isaya 1:10-17 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Sikieni neno la Mwenyezi Mungu, ninyi watawala wa Sodoma; sikilizeni Torati ya Mungu wetu, enyi watu wa Gomora! Mwenyezi Mungu anasema, “Wingi wa sadaka zenu, ni kitu gani kwangu? Nina sadaka za kuteketezwa nyingi kupita kiasi, za kondoo dume na mafuta ya wanyama walionona. Sipendezwi na damu za mafahali wala za wana-kondoo na mbuzi. Mnapokuja kujihudhurisha mbele zangu, ni nani aliyewataka ninyi mfanye hivyo, huku kuzikanyaga nyua zangu? Acheni kuniletea sadaka zisizokuwa na maana! Uvumba wenu ni chukizo kwangu. Miandamo ya Mwezi, Sabato na makusanyiko ya ibada: siwezi kuvumilia makusanyiko yenu maovu. Sikukuu zenu za Miandamo ya Mwezi, na sikukuu zenu zilizoamriwa: moyo wangu unazichukia kabisa. Zimekuwa mzigo kwangu, nimechoka kuzivumilia. Mnaponyoosha mikono yenu katika maombi, nitaficha macho yangu nisiwaone; hata mkiomba maombi mengi sitasikiliza. “Mikono yenu imejaa damu! “Jiosheni na mkajitakase. Yaondoeni matendo yenu maovu mbele zangu; acheni kutenda mabaya. Jifunzeni kutenda mema, tafuteni haki. Wateteeni waliodhulumiwa. Teteeni shauri la yatima, wateteeni wajane.