Hagai 2:10-19
Hagai 2:10-19 BHN
Mnamo siku ya ishirini na nne ya mwezi wa tisa, katika mwaka wa pili wa utawala wa Dario, neno la Mwenyezi-Mungu wa majeshi lilimjia nabii Hagai, akamwambia: “Waambie makuhani watoe uamuzi juu ya jambo hili: Kama mtu akichukua nyama takatifu katika upindo wa vazi lake, kisha akagusa kwa upindo wa vazi hilo mkate au chakula kilichopikwa, au divai, au mafuta au chakula cha aina yoyote ile, je, chakula hicho kitakuwa kitakatifu?” Makuhani wakamjibu, “La, hasha.” Hagai akawauliza tena, “Je, mtu aliye najisi kwa kugusa maiti, akigusa baadhi ya vyakula hivi, chakula hicho kitakuwa najisi?” Makuhani wakamjibu, “Ndiyo, kitakuwa najisi.” Hapo Hagai akawaambia, “Mwenyezi-Mungu asema kwamba, hivyo ndivyo ilivyo kwa watu wa taifa hili na kila kitu wanachofanya; kadhalika na kila wanachotoa madhabahuni ni najisi. “Lakini sasa angalieni mambo yatakayotukia. Kabla ya kuanza kujenga upya hekalu langu, hali yenu ilikuwaje? Mliliendea fungu la nafaka mkitarajia kupata vipimo ishirini, lakini kulikuwa na vipimo kumi tu. Mliliendea pipa la divai mkitarajia kujaza vyombo hamsini, lakini mlikuta ishirini tu. Niliwapiga kwa ukame, ukungu na mvua ya mawe, nikaharibu kila mlichojaribu kupanda, lakini hata hivyo hamkunirudia. Nasema mimi Mwenyezi-Mungu. Leo ni siku ya ishirini na nne ya mwezi wa tisa, siku ambayo msingi wa hekalu umekamilika. Basi, ngojeni mwone yale yatakayotokea tangu leo. Ingawa sasa hamna nafaka ghalani, nayo mizabibu, mitini, mikomamanga na mizeituni haijazaa kitu, lakini tangu leo, nitawabariki.”