Hagai 2:10-19
Hagai 2:10-19 SRUV
Siku ya ishirini na nne, ya mwezi wa tisa, katika mwaka wa pili wa Dario, neno la BWANA lilikuja kwa kinywa cha nabii Hagai, kusema, BWANA wa majeshi asema hivi, Waulizeni sasa makuhani kuhusu sheria, mkisema, Mtu akichukua nyama takatifu katika upindo wa nguo yake, naye kwa upindo wake akagusa mkate, au ugali, au divai, au mafuta, au chakula chochote, je, Kitu hicho kitakuwa kitakatifu? Makuhani wakajibu, wakasema, La. Ndipo Hagai akasema, Kama mtu aliyetiwa unajisi kwa kugusa maiti, akigusa kimojawapo cha vitu hivi, je, Kitakuwa najisi? Makuhani wakajibu, wakasema, Kitakuwa najisi. Ndipo Hagai akajibu, akasema, Hivyo ndivyo walivyo watu hawa, na hivyo ndivyo lilivyo taifa hili mbele zangu, asema BWANA; na hivyo ndivyo ilivyo kila kazi ya mikono yao; na kitu hicho wakitoacho sadaka huko ni najisi. Na sasa nawaomba, tafakarini; tangu siku hii na siku zilizopita; kabla jiwe halijatiwa juu ya jiwe katika nyumba ya BWANA; katika wakati huo wote, mtu alipofikia rundo la vipimo ishirini, palikuwa na vipimo kumi tu; na mtu alipofikia pipa kubwa apate kuteka divai ya vyombo hamsini, palikuwa na divai ya vyombo ishirini tu. Niliwapiga kwa ukavu, na ukungu, na mvua ya mawe, katika kazi zote za mikono yenu; lakini hamkunirudia mimi, asema BWANA. Tafakarini, nawaomba; tangu siku hii ya leo na siku zijazo; tangu siku ya ishirini na nne ya mwezi wa tisa, naam, tangu siku hiyo ulipowekwa msingi wa hekalu la BWANA tafakarini haya. Je, Mbegu ingali ghalani? Naam, huo mzabibu, wala mtini, wala mkomamanga, wala mzeituni, haikuzaa kitu; tangu siku hii ya leo nitawabariki.