Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 47:13-26

Mwanzo 47:13-26 BHN

Baadaye chakula kiliadimika kabisa nchini kote. Njaa ilikuwa kali sana hata ikawafanya watu wote katika nchi ya Misri na ya Kanaani kudhoofika. Yosefu akakusanya fedha yote ya nchi ya Misri na Kanaani kutokana na nafaka waliyonunua, akaipeleka fedha hiyo ikulu kwa Farao. Baada ya watu wote wa nchi ya Misri na Kanaani kutumia fedha yao yote Wamisri wote walimjia Yosefu na kumwambia, “Tupe chakula! Kwa nini tufe mbele ya macho yako? Tazama, sasa fedha yetu imekwisha!” Yosefu akawaambia, “Kama fedha yenu imekwisha, basi nipeni mifugo yenu, nami nitawapa nafaka.” Ndipo wakamletea Yosefu mifugo yao: Farasi, ng'ombe, kondoo, mbuzi na punda, naye akawapa chakula. Mwaka huo Yosefu akawa anawapa chakula kwa kubadilishana na mifugo yao yote. Mwaka uliofuata wakamjia tena na kumwambia, “Bwana, ukweli ni kwamba fedha yetu yote imekwisha, na wanyama wetu wamekuwa mali yako. Sasa, bwana, sisi watumishi wako hatuna chochote tunachoweza kukupa isipokuwa miili yetu na mashamba yetu. Ya nini sisi tufe mbele ya macho yako na mashamba yetu yaharibike? Utununue sisi pamoja na mashamba yetu, tuwe watumwa wa Farao, mradi tu utupe chakula. Tupe nafaka, tusije tukafa; utupe na mbegu kwa ajili ya mashamba yetu.” Hivyo Yosefu akainunua nchi yote ya Misri iwe mali ya Farao. Kila Mmisri alilazimika kuuza shamba lake, kwa jinsi njaa ilivyokuwa kali. Nchi yote ikawa mali ya Farao, na Yosefu akawafanya watu kuwa watumwa, kutoka pembe moja hadi pembe nyingine ya nchi ya Misri. Ardhi ambayo Yosefu hakuinunua ni ile iliyomilikiwa na makuhani. Hao hawakulazimika kuiuza ardhi yao kwani waliishi kwa posho maalumu waliyopewa na Farao. Kisha Yosefu akawaambia watu, “Tazameni, nimekwisha wanunua nyinyi nyote na mashamba yenu kuwa mali ya Farao. Mtapewa mbegu nanyi mtapanda mashamba yenu. Wakati wa mavuno, sehemu moja ya tano mtampa Farao. Sehemu nne zitakazobaki zitakuwa mbegu na chakula kwa ajili yenu na jamaa zenu na watoto wenu.” Wakamjibu, “Bwana, umeyaokoa maisha yetu! Kwa vile umetuonesha wema wako, sisi tutakuwa watumwa wa Farao.” Ndivyo Yosefu alivyotangaza sheria moja ambayo iko mpaka leo nchini Misri: Kila raia lazima atoe sehemu moja ya tano ya mavuno yake kwa Farao. Ardhi ya makuhani tu ndiyo haikununuliwa na kufanywa mali ya Farao.

Soma Mwanzo 47

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Mwanzo 47:13-26