Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 47:13-26

Mwanzo 47:13-26 NEN

Hata hivyo, hapakuwepo chakula katika sehemu yote kwa kuwa njaa ilikuwa kali sana; Misri na Kanaani zote zikaharibiwa kwa sababu ya njaa. Yosefu akakusanya fedha zote zilizopatikana kutoka mauzo ya nafaka huko Misri na Kanaani, akazileta kwenye jumba la kifalme la Farao. Fedha za watu wa Misri na Kanaani zilipokwisha, Wamisri wote wakamjia Yosefu na kumwambia, “Tupatie chakula. Kwa nini tufe mbele ya macho yako? Fedha zetu zimekwisha.” Yosefu akawaambia, “Basi leteni mifugo yenu, nitawauzia chakula kwa kubadilisha na mifugo yenu, kwa kuwa fedha zenu zimekwisha.” Kwa hiyo wakaleta mifugo yao kwa Yosefu, naye akawapa chakula kwa kubadilishana na farasi zao, kondoo na mbuzi zao, ngʼombe na punda zao. Katika mwaka huo wote Yosefu akawapa chakula kwa kubadilishana na mifugo yao yote. Mwaka ule ulipokwisha, wakamjia mwaka uliofuata na kumwambia, “Hatuwezi kuficha ukweli mbele za bwana wetu kwamba, kwa kuwa fedha zetu zimekwisha na wanyama wetu ni mali yako, sasa hakuna chochote kilichosalia kwa ajili ya bwana wetu isipokuwa miili yetu na ardhi yetu. Kwa nini tuangamie mbele ya macho yako, sisi pamoja na nchi yetu? Utununue sisi pamoja na ardhi yetu ili kubadilishana kwa chakula. Nasi pamoja na nchi yetu tutakuwa watumwa wa Farao. Tupe sisi mbegu ili tuweze kuishi wala tusife, nchi yetu isije ikawa ukiwa.” Kwa hiyo Yosefu akamnunulia Farao nchi yote ya Misri. Wamisri, mmoja baada ya mwingine, waliuza mashamba yao, kwa sababu njaa ilikuwa kali sana kwao. Nchi ikawa mali ya Farao, naye Yosefu akawafanya watu watumike kama watumwa, kuanzia upande mmoja wa Misri hadi upande mwingine. Hata hivyo, hakununua nchi ya makuhani, kwa sababu walikuwa wanapata mgawo wao wa kawaida kutoka kwa Farao, nao walikuwa na chakula cha kuwatosha kutokana na mgawo waliopewa na Farao. Hii ndiyo sababu hawakuuza ardhi yao. Yosefu akawaambia watu, “Kwa vile nimewanunua ninyi pamoja na nchi yenu leo kuwa mali ya Farao, hapa kuna mbegu kwa ajili yenu ili mweze kuziotesha. Lakini wakati mazao yatakapokuwa tayari, mpeni Farao sehemu ya tano. Sehemu hizo nne zitakazobaki mtaziweka kama mbegu kwa ajili ya mashamba na kwa ajili ya chakula chenu wenyewe na cha watu wa nyumbani mwenu na watoto wenu.” Wakamwambia, “Umeokoa maisha yetu. Basi na tupate kibali mbele ya macho ya bwana wetu; tutakuwa watumwa wa Farao.” Basi Yosefu akaiweka iwe sheria kuhusu nchi ya Misri, ambayo inatumika mpaka leo, kwamba, sehemu ya tano ya mazao ni mali ya Farao. Ni nchi ya makuhani tu ambayo haikuwa ya Farao.

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Mwanzo 47:13-26