Mwanzo 16:1-6
Mwanzo 16:1-6 BHN
Basi, Sarai, mkewe Abramu, alikuwa bado hajamzalia mumewe mtoto. Lakini alikuwa na mjakazi aliyeitwa Hagari, kutoka Misri. Basi, Sarai akamwambia Abramu, “Unajua kuwa Mwenyezi-Mungu hajanijalia kupata watoto. Mchukue Hagari mjakazi wangu; huenda nikapata watoto kwake.” Abramu akakubali shauri la Sarai. Kisha, Sarai akampa Abramu Hagari, mjakazi wake ambaye alikuwa Mmisri, awe mke wake. Haya yalitokea baada ya Abramu kukaa katika nchi ya Kanaani kwa muda wa miaka kumi. Abramu akamchukua Hagari, naye Hagari akapata mimba. Lakini mara tu alipoona amepata mimba, Hagari akaanza kumdharau bimkubwa wake. Sarai akamwambia Abramu, “Wewe utawajibika kwa ubaya ninaotendewa. Mimi nilikupa mjakazi wangu, lakini alipopata mimba, mimi nimekuwa duni machoni pake! Mwenyezi-Mungu na ahukumu kati yako na mimi!” Lakini Abramu akamwambia Sarai, “Mjakazi wako yuko chini ya mamlaka yako; mfanyie upendavyo.” Basi, Sarai akamtesa Hagari mpaka akatoroka.